Hatimaye, Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika serikali ya awamu ya nne Hayati. Benard Kamilius Membe umepumzishwa, leo tarehe 16 Mei, 2023 katika nyumba yake milele kwenye eneo yalipo makaburi ya familia kijijini Chiponda, Tarafa ya Rondo iliyopo katika Halmashauri ya Mtama, Mkoani Lindi.
Katika hafla ya misa takatifu ya mazishi ya Hayati. Membe iliyoongozwa na Kaimu Naibu Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Padre. Silvanus Kessy na upande wa serikali ukiwakilishwa na Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa {Mb} Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akitoa salamu za rambirambi Leo, Jumanne Mei 16,2023 alipomuwakilisha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa serikali ya awamu ya sita itaendelea kuenzi mchango mkubwa wa Hayati Membe katika serikali ikiwemo ushiriki wake katika vita ya Kagera na ndani ya Chama cha Mapinduzi ambao aliufanya enzi za uhai wake.
“Watanzania, Wananchi wa Lindi na wa hapa Rondo, Mhe, Rais amewataka muenzi yale yote mema aliyoyatenda Hayati Membe wakati wa uhai wake lakini pia endeleeni kumuombea ili Mungu amlaze mahali pema.”
Waziri Mkuu ameendelea kueleza kuwa Rais Dkt. Samia amesema kifo cha Benard Membe kimewaacha Watanzania na wanaLindi kiujumla wakiwa na butwaa kubwa, simanzi na huzuni, “Rais amesema anatoa pole sana kwa wote walioguswa na msiba huu mzito ndani na nje ya nchi yetu”
Aidha, Waziri Mkuu ameeleza kuwa Marehemu Membe atakumbukwa kwa mengi na Watanzania na jumuiya za kimataifa kutokana na utumishi wake uliotukuka katika nafasi mbalimbali alizozihudumia enzi za uhai wake “Marehemu Membe atakumbukwa kwa usikivu wake, upole na weledi katika kufanya kazi na majukumu yake, uzalendo katika taifa na mwenye misimamo thabiti katika yale aliyoyaamini.”
Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa, amehaidi kutoa kiasi cha Tsh. Mil 10 kwa ajiri ya kumalizia marekebisho madogo ya kanisa la Mt. Yohane Mbatizaji, ambalo awali lilipangwa kubarikiwa mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, lakini Marehemu aliomba lifanyiwe marekebisho hivyo linatarajiwa kufunguliwa Agosti, mwaka huu.
Kwa upande wake Raisi mstaafu wa awamu ya nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema alimfahamu Membe kama rafiki wa karibu, MwanaDiplomasia mbobezi, Mwanamikakati makini na mchumi mzuri na alifanya nae kazi katika kipindi cha utawala wake kwa miaka 9 akiwa kama Waziri wa Mambo ya Nje ambapo alifanya kazi kubwa ya kuendeleza maslahi ya Tanzania katika medani za Kimataifa na kikanda.
“Nimemfahamu Membe tangu mwaka 1984, alikua ni mtu makini, mwanadiplomasia na hakua muoga wa kutoa maoni yake tofauti na watu wengine, kama taifa tumempoteza mtu muhimu aliyekua mshauri na aliyesaidia watu mbalimbali bila ya kujali tofauti za itikadi zao, alikua ni mcha Mungu kwelikweli asiyebagua dini ya mtu mwingine na ndio maana hapa Chiponda alijenga Kanisa Katoliki pamoja na Msikiti katika kipindi chote cha uhai wake”
Hayati Benard Kamilius Membe atakumbukwa sana na WanaRondo kwa mchango wake mkubwa katika kuchangia maendeleo ya kijiji chao ikiwemo kusogeza huduma za afya na elimu kwa wananchi hao, huduma za maji safi, barabara pamoja na ujenzi wa ofisi za uongozi wa kijiji hicho.
RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA, NA MWANGA WAKO UMUANGAZE.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.