Kauli Mbiu: “Tumia Taaluma Yako, Tokomeza Vifo vya Mama Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto Wachanga.”
Mkoa wa Lindi unaendelea na harakati za kuhakikisha kuwa vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga vinapungua hadi kufikia dijiti moja.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi Dkt. Kheri Kagya katika hafla fupi ya kuhitimisha kikao kazi cha siku tatu cha kujadili Vifo vitokanavyo na Uzazi na Watoto wachanga ngazi ya Mkoa kilichokutanisha timu ya wataalamu Wasimamizi wa Afya ngazi za Halmashauri na Mkoa (CHMT na RHMT)
"Tuna kila sababu ya kujivunia mafanikio tunayoendelea kuyapata katika mapambano dhidi ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga, na hii ni kutokana na uwajibikaji wa uongozi na watendaji katika sekta ya afya. Takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia mwezi Jan hadi Juni 2025 tuna vifo 9 tu Mkoa mzima" Dkt. Kagya
Akimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Ndugu. Nathalis Linuma ameeleza kuwa tathmini imeonyesha ongezeko la akinamama wanaojifungua katika vituo vya afya kutoka 96% mwaka 2021 hadi 98% mwaka 2024 na kueleza kuwa ongezeko hilo ni ishara nzuri, na kuwataka wataalamu kuboresha na kujikita kutoa huduma bora za afya kwa mama na mtoto.
Aidha, Ndugu. Linuma amewataka wataalamu kuhakikisha kuwa wajawazito wanapata elimu ya umuhimu wa kuhudhuria kliniki katika miezi ya awali ya ujauzito ili kufikia lengo la serikali la 60%.Huku akisisitiza umuhimu wa kuwatumia watoa huduma za afya ngazi ya jamii CHW kuelimisha na kushawishi wanajamii juu ya umuhimu wa hudhurio la awali kwa wajawazito.
Bi. Sophia Mchinjita, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Kanda ya Kusini amepongeza uratibu wa zoezi la uchangiaji na ukusanyaji wa damu salama unaofanywa na Mkoa, ambapo mwaka 2024 Mkoa wa Lindi umekua kinara katika zoezi la uchangiaji.
Bi. Mchinjita ameongeza kuwa damu zinazokusanywa zinatumika kwa akiba inapotokea dharura ya mama anayejifungua kupoteza damu nyingi na kwa watoto wachanga wanaozaliwa na changamoto hiyo hivyo kuokoa maisha.
Aidha, amezipongeza Halmashauri za Kilwa na Mtama kwa kupunguza kwa kasi vifo vya mama na mtoto ambapo kwa mwaka huu Halmashauri ya Kilwa imeripoti kifo 1 tu, ukilinganisha na awali ambapo ilikua inaongoza kwa kuwa na vifo vingi vitokanavyo na uzazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.