MWEKEZAJI WA KIWANDA CHA KUCHAKATA MABAKI YA NAZI NA MAGANDA YA KOROSHO ASAINI MKATABA LINDI.
Leo, Novemba 13, 2025, Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na raslimali watu Ndugu Nathalis Linuma, ameongoza kikao cha kusaini makubaliano ya mkataba wa uwekezaji kati ya Serikali ya Mkoa wa Lindi na kampuni ya African Coconut Material Production (ACMP) kutoka China, ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bwana Wang Hai Peng.
Mkataba huo, wenye thamani zaidi ya bilioni 1.2, unahusu uwekezaji wa kiwanda kitakachojengwa katika eneo lenye ukubwa wa Mita za Mraba 46,855 lililopo Kijiji cha Mtange, mkoani Lindi.
Ujenzi wa kiwanda hicho unatarajiwa kuanza mwezi Novemba 2025 na kukamilika Novemba 2026. Mara baada ya kukamilika, kiwanda kitajikita katika kusindika na kuchakata mabaki ya nazi na maganda ya korosho ili kuzalisha mkaa.
Kupitia uwekezaji huu, wananchi wa Mkoa wa Lindi wanatarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa kupitia upatikanaji wa ajira ambapo zaidi ya vijana 200 wazawa wanatarajiwa kuajiriwa katika kiwanda hicho,jambo litakalosaidia kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira katika mkoa wa Lindi. Aidha, kampuni ya ACMP kwa kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa, itatoa elimu kwa wakulima wa maeneo yote wanaozalisha mazao hayo juu ya mbinu bora za kilimo na utunzaji wa mabaki ya mazao hayo ili kuongeza tija na thamani ya mazao kwa kutengeneza mnyororo wa thamani kupitia maganda ya korosho na mabaki ya nazi.







Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.