Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omary amewataka wajasiriamali wadogo kuwa wabunifu katika bidhaa wanazozizalisha ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifungashio bora vinavyoendana na mahitaji ya soko ili kukuza wigo wa masoko.
Bi. Zuwena ameyasema hayo wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la Wafanyabiashara ndogondogo Mkoa wa Lindi lenye Kauli Mbiu isemayo "Ubunifu na Ushirikiano ni njia ya Mafanikio kwa wafanyabiashara ndogondogo"
Katibu Tawala amesema kuwa serikali inaendelea kutenga maeneo kwa ajiri ya kuanzisha viwanda vidogo vya uzalishaji na uchakati wa bidhaa mbalimbali kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo SIDO ili kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali kufanya shughuli zao na kufuatiliwa kwa karibu ili waweze kukua na kusisitiza kuwa ushirikiano baina yao ni nyenzo muhimu ya kufikia maendeleo wanayoyataka.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwa maandalizi ya kongamano hilo na ushiriki wao katika kuhakikisha makundi maalumu yanapata fursa stahiki na kuzitaka Halmashauri za Mkoa wa Lindi kuendelea kuwatambua wajasiriamali hao kwa kuwasajiri na kuwapatia vitambulisho vitakavyowatambulisha katika fursa mbalimbali na kushirikiana na taasisi za kifedha ili kuwapa elimu ya usimamizi wa fedha pamoja na huduma za mikopo itakayowawezesha kuinua vipato vyao.
Bi. Zuwena amewahimiza wajasiriamali kujitokeza kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika ifikapo Oktoba ili wapate nafasi ya kuchagua viongozi wataotetea maslahi yao na kuwausia kutojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani katika kipindi chote cha uchaguzi.
Kongamano la Wafanyabiashara ndogomdogo limefanyika leo Agosti 25, katika ukumbi wa mkutano Dockyard katika Halmshauri ya Manispaa ya Lindi na kukutanisha makundi maalumu ya wafabya biashara ndogondogo wakiwemo wajasiriamali wadogo, wamachinga, wasusi, washonaji, waendesha bodaboda, bajaji na guta, baba na mama lishe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.