Katika kuhakikisha Taifa linajengwa kwa misingi imara ya maendeleo endelevu, vijana wametakiwa kuwa wabunifu, wachapa kazi, waadilifu na wavumilivu. Haya yamesemwa kama sehemu ya wito kwa vijana kuacha kusubiri kufanyiwa bali kujitokeza na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii zao.
Wito huo umetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dkt. Henry Kagya, alipokuwa akizungumza na vijana wa kada mbalimbali katika maadhimisho ya Siku ya Vijana 2025, yaliyofanyika katika Manispaa ya Lindi.
Dkt. Kagya amesema kuwa ili vijana waweze kutekeleza majukumu hayo ipasavyo, ni muhimu wajali afya zao, kwani afya bora ni msingi wa uzalishaji na mchango wa maana kwa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Bi. Rahma Dadi, Mshauri Mwandamizi wa Mambo ya Vijana na Jinsia kutoka mradi wa USAID Afya Yangu – Southern Project, amesema kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Matendo ya Vijana kwa Maendeleo Endelevu Zaidi” inasisitiza umuhimu wa vijana kuchukua hatua chanya zitakazosaidia kuleta maendeleo.
Bi. Rahma ameongeza kuwa kwa kutambua umuhimu huo, waliamua kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi – Sokoine kuandaa maadhimisho hayo katika eneo hilo la hospitali, kwa lengo la kuwapa vijana fursa ya kujifunza na kufahamu mambo mbalimbali kuhusu afya, uongozi, na fursa za maendeleo kutoka kwa wadau tofauti.
Naye Polisi Constable Adam, kutoka Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Lindi, alitumia jukwaa hilo kuwakumbusha vijana kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, akisisitiza kuwa matumizi hayo si tu yanaharibu afya bali pia yanadhoofisha uchumi wa taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.