Mkoa wa Lindi unatajwa kuwa kinara wa uzalishaji wa zao la mwani wenye ubora zaidi miongoni mwa mikoa inayopakana na mwambao wa bahari ya hindi ambapo wazalishaji na wachakataji wakuu wa zao hilo wakiwa ni wajasiriamali wanawake ambao kwa sasa kilio chao kikuu ni kuwezeshwa upatikanaji wa viwanda vitakavyowawezesha kuchakata zao hilo ili kuweza kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi kwa ufanisi.
Wajasiriamali hao wakiwezeshwa wanaweza kumudu kuhudumia soko la ndani pamoja na kuweka ushindani katika bidhaa zitokanazo na mwani katika masoko ya kimataifa.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack alipokua akifanya mahojiano maalumu na Watangazaji wa Kituo cha Uhuru Fm kuhusu Gulio la Bidhaa za Usindikaji na Ushonaji lililozinduliwa Mkoani Lindi Novemba 2 na Mhe. Dkt. Seleman Jafo (Mb) Waziri wa Viwanda na Biashara.
"Lengo la gulio ni kufungua fursa za kibiashara na kutoa nafasi ya wajasiriamali kujitangaza ili kujisogeza karibu kwa wanunuzi na tunashukuru kwa mwanzo huu maana tumeona milango ya fursa imefunguka na wajasiriamali wetu wameanza kunufaika kutokana na kile wanachokifanya" Ameeleza
"Tukiwa kama wazalishaji wa kwanza wa zao la mwani tumedhamiria kujitangaza ili watu wafahamu kuhusu ubora wa mwani unaolimwa Lindi, mwani halisi unaotoka baharini, kuanikwa kwa kuzingatia viwango na kusagwa bila kuongezwa kitu chochote hivyo kufaa kwa matumizi ya chakula cha binadamu na ndio maana tumemuomba Waziri wa Viwanda kutusaidia kupata viwanda vitakavyowawezesha wajasiriamali wetu kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi"
Zao la Mwani linatajwa kuwa miongoni mwa mazao bora zaidi lenye madini mengi yanayohitajika katika ustawi wa mwili wa binadamu na hutumika zaidi kwa matumizi ya chakula, dawa ya kutibu maradhi mbalimbali na kutengenezea vipodozi vya asili kwa ajiri ya nywele na ngozi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.