Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi, kwa kushirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, imefanya ziara rasmi ya kukagua na kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Nachingwea.
Ziara hiyo imefanyika Februari 11, 2026, ikiongozwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Lindi, Ndg. Barnabas Y. Essau, akiwa ameambatana na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ndg. Juhudi Mgallah, Katibu Tawala – Sehemu ya Mipango na Uratibu. Aidha, ziara hiyo ilihusisha Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Mohamed Moyo, Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Lindi, Wajumbe wa Kamati ya Siasa ngazi ya Wilaya, pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.
Baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali, Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Lindi imepongeza kasi, ubora na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.6, ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM inayolenga kuwaletea wananchi maendeleo endelevu na kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi.
Kamati hiyo imekagua Mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3, ujenzi wa barabara ya lami kutoka KKKT hadi Hospitali ya Wilaya unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 356; pamoja na mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Msingi na Awali katika eneo la Shule ya Sekondari Stesheni wenye thamani ya shilingi milioni 314.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu madhubuti na endelevu wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo unaolenga kuimarisha uwajibikaji na uwazi, kuongeza ufanisi na kasi ya utekelezaji, pamoja na kuhakikisha kuwa miradi hiyo inaleta matokeo chanya, yenye tija na manufaa ya kudumu kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea.




Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.