Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, amemsifu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake kubwa katika kuleta maendeleo, akimtaja kama "Rais wa Kujenga Taifa."
Akizungumza Machi 15 katika Mkutano wa Diwani wa Ilani uliofanyika Kata ya Narungombe, wilayani Ruangwa, Mhe. Telack alieleza kuwa Rais Samia ameleta miradi mingi inayoboresha maisha ya wananchi wa Lindi.
Amefafanua kuwa Kata ya Narungombe pekee imepokea miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 7.8, ikijumuisha sekta ya elimu, afya, maji, na miundombinu. Mhe. Telack amesema fedha hizo ni uthibitisho wa dhamira ya Rais Samia katika kuinua maisha ya wananchi na kuimarisha huduma muhimu vijijini.
Aidha, Mhe. Telack amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kupongezwa na wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wote bila ubaguzi.
"Tunaona miradi ya shule, zahanati, barabara, na maji inatekelezwa kwa kasi kubwa. Huu ni ushahidi tosha kwamba Rais wetu ni kiongozi wa vitendo na anayeweka maendeleo mbele," amesema Mhe. Telack.
Pia, Mhe. Telack amehitimisha kwa kusema kuwa Mkoa wa Lindi utaendelea kushirikiana na Serikali ya Rais Samia kuhakikisha miradi yote inaenda sambamba na mahitaji ya wananchi, huku akiwahimiza wananchi waendelee kuwa na mshikamano na kujitokeza kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.