Wizara ya Sheria na Katiba imeendesha kikao cha mafunzo na Wataalam wataoshiriki katika utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria Mkoani Lindi kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campgain) yenye lengo la kutoa elimu mbalimbali za Kisheria pamoja na utatuzi wa migogoro.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bwana. Nathalis Linuma ametoa rai kwa washiriki wa kikao hicho kuzingatia na kutumia mafunzo hayo kama chachu na mwangaza wa kuwasaidia wananchi kwa kuwapatia huduma za msaada wa kisheria katika kipindi cha kampeni.
"Ni matarajio yangu kuwa mtafata mwongozo wa utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia utakaotolewa na wataalam wa Wizara ili kuhakikisha kampeni inawanufaisha walengwa hususan wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili, ni vyema kuhakikisha kila mwananchi anaguswa na kampeni hii ili kwa pamoja tuweze kupunguza na kuondoa migogoro hususan ya kisheria inayowakabili wananchi"
Aidha, Bwana. Linuma amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo ya mikutano ili waweze kupata fursa ya kujifunza kuhusu masuala ya kisheria na kupata nafasi ya kuwasilisha mashauri yao ya kisheria ili kupata ufumbuzi na utatuzi wa shauri husika kwa usahihi.
Kwa upande wake Mkurugenzi na Msajiri wa Watoa Huduma za Kisheria Bi. Ester Msambazi ameeleza kuwa Kampeni hii inatekelezwa katika Mikoa 26 yaTanzania bara na 5 ya Tanzania visiwani ambapo kati ya hiyo Mikoa 17 tayari imeshafikiwa.
"Uwepo wa kampeni hii umetokana na ombwe kubwa la kisheria lililopo miongoni mwa wanajamii hivyo kampeni imekuja kuleta uelewa wa masuala ya kisheria na elimu ya sheria miongoni mwa wananchi pamoja na kutoa huduma ya msaada wa kisheria inayohusu usuluishi nanutatuzi wa migogoro ikiwemo ya ardhi, jinai na madai pamoja na masuala ya mirathi na wosia"
Msaidizi Msaidizi wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Lindi, Joyce Kitesho ameeleza kuwa wanatarajia kampeni hii itakua ni chachu ya kupunguza migogoro mingi inayotokana na ukatili wa kijinsia ambayo waathirika wake wakuu ni wanawake na watoto kutokana na ukosefu wa elimu ya kisheria kunakopelekea waathirika kukosa haki zao panapotokea migogoro.
Kampeni ya Utoaji wa Huduma ya Msaada wa Kisheria itaendeshwa kwa muda wa siku 9 katika Halmashauri zote za Mkoa wa Lindi kuanzia Februari 19 hadi Februari 28, 2025 ambapo elimu mbalimbali zinazohusu masuala ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pamoja na utatuzi wa migogoro ikiwemo ya ardhi, mirathi, wosia, madai na jinai zitatolewa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.