Bi. Madenge awataka wasimamizi wa uchaguzi kusimamia kiapo
Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bi. Rehema Madenge amewataka wasimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa kuhakikisha wanasimamia uchaguzi kwa kuzingatia kiapo, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Bi. Madenge ameyasema hayo wakati wa zoezi la uapishaji wa wasimamizi hao lililofanyika katika ukumbi mdogo wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi ambapo wasimamizi sita (6) wa uchaguzi kutoka halmashauri za mkoa wa Lindi waliapa kiapo mbele ya hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Lindi, Mhe. James Karayemaha na kushuhudiwa na baadhi ya watendaji wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Wasimamizi wametakiwa kutambua kuwa kiapo walicho apa sio cha utani kwani tayari wameshaweka ahadi mbele ya Mungu, serikali na wananchi hivyo endapo watakigeuka sio tu watapata adhabu kwa mujibu wa sheria bali hata kwa Mungu pia wataadhibiwa.
“Nimshukuru sana hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa kwa ufafanuzi mzuri alioutoa kuhusu kiapo kwani kumekuwepo na uelewa mbovu wa kufikiri kuapa ni kitu sha masihara. Niwasihi wasimamizi wote kuhakikisha mnasimama katika kiapo chenu na kutoruhusu kutingishwa na mtu yeyote”, alisema Bi. Madenge.
Bi. Madenge amewataka wasimamizi hao kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi mbalimbali katika maeneo wanayotoka bila kuacha kusimamia misingi ya kiapo, sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi zilizopo ili uchaguzi utakaofanyika ufanyike kwa amani na utulivu.
Naye hakimu mkazi mfawidhi mkoa, Mhe. James Karayemaha amesema kuwa wasimamizi ni lazima watambue kuwa kazi wanayokwenda kuifanya ni nyeti sana kwani inahusu uchaguzi wa viongozi ambao watawaongoza wananchi kwa miaka mitano (5). Hivyo ni lazima watambue kuwa wao ndio chanzo cha utawala bora na chanzo cha maendeleo.
Mhe. Karayemaha amewasihi wasimamizi kutokuwa chanzo cha kuharibu uchaguzi kitu ambacho kitasababisha wao kupelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria na kusababisha serikali kuingia gharama za kuendesha kesi za uchaguzi katika mkoa na wao kuingia katika matatizo ambayo yanaweza wasababishia kufungwa.
Wasimamizi walioapishwa ni Ndg. Mohmoud Alli Kimbokota wa halamashauri ya wilaya ya Lindi, ndg. Michael Henze Maganga wa manispaa ya Lindi, ndg. Damas Mumwi wa halmashauri ya wilaya ya Liwale, ndg. Stephen Martin Pundile wa halmashauri ya wilaya ya Kilwa, ndg. Ally Mnunduma Adballah wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea na ndg. Selemani Amiri Mlope wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasimamizi wameahidi kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia kiapo, sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili uchaguzi uweze kufanyika kwa amani. Wote kwa ujumla wao wanatambua jukumu walilopewa ni zito hivyo wameomba ushirikiano kutoka kwa viongozi, wataalam na wananchi kwa ujumla ili waweze kulifanikisha kwa ufanisi.
Picha mbalimbali za uapisho ambapo kuanzia picha ya kwanza ni ndg. Stephen Martin Pundile wa halmashauri ya wilaya ya Kilwa, ndg. Mohmoud Alli Kimbokota (Lindi DC), ndg. Michael Henze Maganga (Lindi MC), ndg. Damas Mumwi (Liwale DC), ndg. Ally Mnunduma Adballah (Nachingwea DC) na ndg. ndg. Selemani Amiri Mlope (Ruangwa DC) na wengine ni wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakishuhudia zoezi la uapisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.