RAS LINDI ATOA MAAGIZO 7 KWA MAAFISA
MAENDELEO YA JAMII.
~Asisitiza Uwazi, Uwajibikaji na Utekelezaji.
Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri za Mkoa wa Lindi leo tarehe 04 Disemba 2025 wamekutana katika Kikao Kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Dockyard, Lindi Manispaa, chenye lengo la kujenga uwezo na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao katika sekta ya maendeleo ya Jamii.
Akizungumza katika kikao hicho, Mgeni Rasmi ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary, ameeleza kuwa serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kuchochea maendeleo ya wananchi na kuboresha ustawi wa jamii. Ameeleza kuwa kazi wanazozifanya zimeendelea kuleta matokeo chanya, ingawa bado yapo maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu ili kuongeza tija na ufanisi katika ngazi zote.
Katika hotuba yake, Bi. Zuwena ametoa maagizo mahsusi kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii ili kuimarisha uwajibikaji, ufuatiliaji na utoaji wa huduma kwa wananchi. Ameelekeza kuimarishwa kwa ufuatiliaji wa vikundi vinavyodaiwa mikopo ya asilimia 10 kwa lengo la kusimamia marejesho, kuanzishwa kwa majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika ngazi za kata, pamoja na kuimarishwa kwa mabaraza ya watoto yenye kufanya kazi kikamilifu kuanzia ngazi ya jamii.
Amesisitiza pia umuhimu wa utoaji endelevu wa elimu ya lishe, uundaji wa kamati za kupinga ukatili wa kijinsia katika ngazi za kata na wilaya pamoja na kuhakikisha vikao vya robo mwaka vinafanyika kwa mujibu wa mwongozo. Aidha, amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na miongozo ya utumishi wa umma, huku wakihamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika kuchangia na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Bi. Zuwena amesema hatua ya serikali kuunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inalenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa jamii na kuhakikisha wataalamu wa sekta hiyo wanatambulika na kuthaminiwa.
Amewahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuunga mkono jitihada hizo kwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwazi na kuzingatia dhamira ya serikali ya kuwatumikia wananchi.





Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.