DC MWANZIVA AKABIDHI VIFAA VYA MIL 179 UWEZESHAJI WAKULIMA WA MWANI LINDI.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mh. Victoria Mwanziva, leo Oktoba 21, 2025, amekabidhi vifaa vya uwezeshaji wakulima wa zao la mwani katika kijiji cha Shuka, kata ya Navanga, Halmashauri ya Mtama vyenye thamani ya Shilingi Milioni 179. Ikiwa hafla hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), kwa kushirikiana na Agriculture and Fisheries Development Program (AFDP).
Akizungumza katika hafla hiyo, Mratibu wa mradi huo, Ndugu Salim Mwijaga, alisema AFDP imekuwa ikitekeleza miradi ya kuwawezesha wananchi katika sekta za kilimo na uvuvi ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kupitia ushirikiano huo, Serikali imefanikisha ugawaji wa vifaa mbalimbali kwa wakulima wa mwani katika vijiji vinne vya Shuka, Mmumbu, Mongomongo na Sudi.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na boti, chachacha, kamba kubwa na ndogo, kofia za usalama na glovu, ambavyo vinalenga kuboresha shughuli za kilimo cha mwani na kuongeza tija kwa wakulima.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya amesema Serikali itaendelea kuwezesha wakulima kupitia utoaji wa elimu, matumizi ya teknolojia za kisasa, pamoja na ushirikiano na wadau mbalimbali ili kukuza uzalishaji wa zao hilo muhimu na kuleta maendeleo ya kiuchumi nchini.
“Juhudi hizi zinazotekelezwa na Mh. Dkt. Samia suluhu, ambaye ni raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni moja ya utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi katika kukuza uchumi wa nchi, kupitia sekta hii ya uvuvi na uchumi wa blue ni sekta muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. Tukio la leo la kukabidhi vifaa na Boti vitavyotumika kulimia mwani katika halmasharui ya mtama ni sehemu ya mkakati wa serikali kuhakikisha uzalishaji wa zao la mwani unaongezeka. Hatua hii inalenga kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa vifaa na usafirishaji wa mwani kutoka shambani hadi maeneo ya kukaushia . Maboresho haya yatasaidia kuongeza tija na thamani ya zao la mwani, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakulima na jamii kiujumla” Amesema Mhe. Mwanziva.
Vifaa hivyo vitasaidia kuboresha shughuli za kilimo cha mwani kwa kurahisisha usafiri wa wakulima kufika mashambani, kuongeza usalama wakati wa kazi, na kupunguza gharama za uzalishaji. Zao la mwani limeendelea kuwa chanzo kikuu cha kipato kwa wananchi wengi wa eneo hilo.
Mmoja wa wakulima wa kijiji cha Shuka, Bi. Zuwena Sudi yusuph ameishukuru Serikali na wadau kwa msaada huo akisema:
“Tunaishukuru Serikali pamoja na wadau kwa kutupatia vifaa hivi. Awali tulikuwa tunapata shida ya usafiri kufika mashamba, sasa tumepata boti ambayo itarahisisha safari. Pia tulikuwa tunakosa kamba, lakini sasa tumepatiwa. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuona na kutuunga mkono.” Amesema Bi. Zuwena.
Kupitia kilimo cha mwani, wakulima wamekuwa wakipata kipato kinachowawezesha kukidhi mahitaji muhimu ya kijamii kama vile kugharamia elimu za watoto na mahitaji ya kila siku ya familia.



















Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.