Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, amesema Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa maeneo yaliyobarikiwa kuwa na madini ya kila aina, hususani yale ya kimkakati ambayo yana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa.
Dkt. Kiruswa ametoa hayo leo Juni 13, 2025, wakati akiwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Madini na Fursa za Uwekezaji Lindi (Lindi Mining Expo 2025), yanayoendelea katika viwanja vya maonesho ya madini vilivyopo Kilimahewa, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Aidha, Mhe. Dkt Kiruswa amepongeza maandalizi na uratibu wa maonesho hayo kwa kuwaleta pamoja wadau muhimu kutoka sekta mbalimbali, wakiwemo wachimbaji wadogo, wawekezaji wakubwa, taasisi za fedha, na mashirika ya umma na binafsi.
“Lindi imebarikiwa na ni Mkoa tajiri sana una madini ya kimkakati, nawapongeza sana kwa jukwaa hili zuri pia niwapongeze kwa maandalizi mazuri” amesema Dkt. Kiruswa.
Vilevile, ameeleza kuridhishwa na namna mabanda yalivyopangwa na kuwasilisha taarifa za kitaalamu zinazolenga kuhamasisha uwekezaji na matumizi bora ya rasilimali za madini kwa maendeleo jumuishi.
Kwa upande wao, waandaaji wa maonesho hayo wamesisitiza kuwa Lindi Mining Expo ni jukwaa linalolenga kuibua fursa, kuhamasisha ubunifu na kukuza ushirikiano kati ya sekta ya madini na wadau wake katika ngazi zote, huku likitangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana ndani ya Mkoa wa Lindi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.