DKT. SHEKALAGHE AAGIZA HUDUMA KUANZA KUTOLEWA HOSPITALI MPYA YA RUFAA LINDI SOKOINE IFIKAPO JANUARI 1, 2026
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, leo Novemba 26, 2025 amefanya ziara ya kikazi mkoani Lindi ili kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi – Sokoine, inayojengwa katika eneo la Mitwero, Manispaa ya Lindi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Shekalaghe amesema kuwa lengo kuu ni kufuatilia utekelezaji wa mradi huo na kubaini changamoto zinazochelewesha kuanza kutolewa huduma, ili kuhakikisha zinapatiwa majibu ya haraka.
Ameeleza kuwa wananchi wanasubiri kwa hamu kuanza kupata huduma katika majengo mapya ya kisasa. Dkt. Shekalaghe amesema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo umefikia asilimia 98, ikiwa ni pamoja na usimikaji wa vifaa tiba muhimu kama CT-Scan na mashine za kisasa za X-ray.
Amesisitiza kuwa ifikapo Januari 1, 2026, huduma zote lazima ziwe zimehamishiwa rasmi katika hospitali mpya ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji huo mkubwa wa Serikali.
Aidha, Katibu Mkuu ametambua changamoto ya usafiri kwa watumishi wanaotakiwa kufika hospitalini mapema kila siku.
Ameahidi kuwa Wizara italeta basi maalum kwa ajili ya watumishi ili kurahisisha usafiri na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika hospitali hiyo. Pia, Dkt. Shekalaghe amesisitiza umuhimu wa kusogezwa huduma muhimu za kijamii katika eneo linalozunguka hospitali hiyo, ikiwemo upatikanaji wa maji, umeme wa uhakika, maduka, maeneo ya chakula pamoja na makazi salama.
Amesema hatua hizi zitaboresha mazingira kwa watumishi, wagonjwa na ndugu wanaowahudumia. Hata hivyo, amebainisha kuwa Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana kwa karibu na uongozi wa Mkoa wa Lindi na Hospitali ya Sokoine kuhakikisha hospitali hiyo mpya inakuwa kitovu cha huduma za kibingwa na bingwa bobezi.
Lengo likiwa ni kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda mikoa mingine na hivyo kupunguza gharama kwa wananchi.




Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.