Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake katika kusimamia sekta za nishati na maji mijini, kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini yanayofanyika katika Viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi.
Katika maonesho hayo, EWURA ilieleza kuwa ina jukumu la kutoa na kusimamia leseni kwa watoa huduma, kuidhinisha bei za bidhaa kama vile petroli, umeme na gesi asilia, pamoja na kushughulikia migogoro kati ya watoa huduma na wateja kwa njia ya kisheria.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Abdallah Mussa Mwaipaya, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa EWURA, Bwana. Nyiragu Musira, alieleza kuwa moja ya majukumu ya EWURA ni kutatua malalamiko yanayohusu huduma za nishati na maji. Alibainisha kuwa migogoro hiyo hutatuliwa kwa hatua mbili, awali kwa njia ya mazungumzo kupitia maofisa wa huduma kwa wateja, na ikiwa haitapatiwa suluhisho, hupelekwa kwa wanasheria wa EWURA ambapo huchukuliwa kama kesi za mahakamani. Aidha, wateja au watoa huduma wana haki ya kukata rufaa endapo hawaridhishwi na maamuzi ya awali.
Ndugu. Musira ameendelea kueleza kuwa EWURA inaendelea na dhamira yake ya kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kuhakikisha jamii inajiepusha na matumizi ya nishati chafu kama mkaa na kuni ambapo kwa mujibu wa takwimu za EWURA matumizi ya nishati safi nchini yameongezeka hadi kufikia zaidi ya asilimia 30 katika mwaka wa fedha 2023/2024, kutokana na juhudi za serikali na wadau mbalimbali katika kutangaza matumizi hayo.
Aidha, Wananchi wamehimizwa kufika kwenye banda la EWURA kupata elimu zaidi kuhusu haki zao, taratibu za kupata huduma, na namna ya kushughulikia malalamiko dhidi ya watoa huduma. Pia, wadau wa sekta za nishati na maji wametakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka hiyo katika kuwahudumia wateja wao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.