Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Lindi, ikiambatana na wataalam kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, imefanya ziara rasmi ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Ruangwa, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ziara hiyo imefanyika leo, Februari 10, 2026, ikiongozwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Lindi, Ndg. Barnabas Y. Essau, akishirikiana na muwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ndg. Juhudi Mgallah, Katibu Tawala Seksheni ya Mipango na Uratibu.
Katika ziara hiyo, kamati imekagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Chinongwe na kuridhishwa na hatua ya utekelezaji iliyofikiwa.
Kamati imesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati, kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na kuanza kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
Aidha, kamati imetembelea mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Awali na Msingi Kitandi, ambapo imepatiwa taarifa ya maendeleo ya ujenzi pamoja na maandalizi ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia. Kamati imepongeza hatua zilizofikiwa na kusisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji ili mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Vilevile, kamati imekagua mradi wa ujenzi wa barabara za ( Mipingo na Lichonyo) na kupongeza juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, hatua inayochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii. Miradi hiyo yenye thamani zaidi ya Shilingi bilioni 1.
Akizungumza katika kikao cha majumuisho ya ziara hiyo, Ndg. Essau amesema, “Tunawapongeza watendaji wa Halmashauri kwa kazi kubwa iliyofanyika katika utekelezaji wa miradi hii. Ni muhimu kuongeza kasi ya utekelezaji katika maeneo yaliyobaki, kuzingatia ubora wa miradi, na kuhakikisha usimamizi thabiti wa rasilimali ili huduma zilizokusudiwa ziwafikie wananchi kwa ufanisi.” amesema Essau.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu endelevu wa ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo unaolenga kuimarisha uwajibikaji, kuongeza ufanisi wa utekelezaji, na kuhakikisha miradi inaleta matokeo chanya kwa wananchi wa Wilaya ya Ruangwa.




Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.