Mkoa wa Lindi umepokea timu za madaktari bingwa na bingwa bobezi 49 kutoka hospitali mbalimbali za Rufaa ambao wanatarajiwa kutoa huduma za kibingwa na bobezi katika hospitali 7 za Halmashauri za Mkoa wa Lindi kwa muda wa siku tano kuanzia leo Septemba 15 hadi Septemba 19, 2025.
Ujio huu ukiwa ni wa awamu ya nne ya utekelezaji wa azma ya serikali ya kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi pamoja na kutambua wahitaji wa huduma za afya ili kuwapatia rufaa kwa matibabu zaidi, umekua na manufaa zaidi kwani umewezesha mashirikiano baina ya madaktari bingwa na watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya kwakuwa ni darasa la kubadilishana uzoefu na kujenga uwezo wa kiutendaji.
Akizungumzia mafanikio ya Awamu iliyopita, Bwana. Ephraim Kafilimbi, Mratibu wa Huduma za Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi Mkoa wa Lindi amesema kuwa wagonjwa wapatao 230524 waliweza kuhudumiwa pamoja nao wagonjwa 16000 walipata huduma za upasuaji. Vilevile, wahudumu wa afya 15000 katika vituo vya kutolea huduma za afya waliweza kupatiwa mafunzo ya kujiendeleza ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa katika maeneo yao hivyo kutoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kupatiwa huduma kulingana na mahitaji yao.
"Katika Mkoa wa Lindi huduma hizi zinaanza kutolewa kuanzia leo hadi tarehe 19, tutakua tumekamilisha siku tano, kwa madaktari wetu hii ni sehemu endelevu ya kuifanya kazi hii na tuifanye kwa uaminifu ili wananchi wajue kuna wataalamu mabingwa na bobezi wanaoweza kuifanya kazi kwa ubora na wananchi waweze kunufaika na huduma tunazotoa" ameeleza.
Jumla ya Halmashauri 184 za Tanzania Bara zinatarajiwa kufikiwa na Huduma za Madaktari Bingwa na Bingwa bobezi katika awamu hii ya nne ambapo huduma mbalimbali za kibingwa na bobezi zitatolewa katika maeneo ya Magonjwa ya Ndani, Huduma za Ganzi na Usingizi, Magonjwa ya wanawake, Huduma za Uzazi na watoto wachanga, Huduma za Kinywa na Meno pamoja na Huduma za Upasuaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.