KUELEKEA MIAKA 71 YA SOKOINE RRH, MGANGA MKUU WA MKOA AZINDUA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA ITAKAYODUMU KWA SIKU 5.
Kuelekea Maadhimisho ya Miaka 71 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine, Uongozi wa Hospitali hii imeandaa kambi maalumu ya Madaktari Bingwa kutoka hospitali mbalimbali za Rufaa kwa lengo la kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha utoaji wa huduma afya pamoja na kusogeza huduma za afya za kibingwa kwa wananchi. Akimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Lindi katika uzinduzi wa kambi hiyo inayotarajiwa kutoa huduma kwa muda wa siku tano kuanzia leo Jumatatu ya Oktoba 20 hadi Ijumaa Oktoba 24, Katibu Tawala Msaidizi Afya Dkt. Kheri Kagya amewahimiza wananchi umuhimu wa kufatilia mwenendo wa afya zao na kugundua magonjwa yanayowakabili kabla hayajawa sugu mwilini. "Kuna kasumba mbaya miongoni mwetu hususani wanaume, ya kutokuja hospitali hadi tuwe tumezidiwa sana hii hupelekea ucheleweshwaji wa matibabu na kukomaza ugonjwa. Niwasihi wananchi tujenge utamaduni wa kuchunguza afya zetu na kuwahi katika vituo vya matibabu ili tupate huduma kwa wakati na tuendelee kulinda afya zetu na kuepuka kutumia gharama kubwa kwa ajiri ya matibabu" Aidha, Dkt. Kagya amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika Kambi ya Madaktari Bingwa ili kuweza kupata huduma za matibabu ya kibingwa na kusisitiza kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa kuanzia kwenye miundombinu, vifaa tiba, madawa na wataalamu wa afya, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya stahiki katika maeneo yao na kuwapunguzia gharama za kusafiri ili kupata huduma hizo. Bi. Salma Magota, mkazi wa kata ya Wailes ameshukuru ujio wa kambi hii kwani imewapunguzia mzigo wa kupata rufaa kwenda maeneo mengine. "Tumefurahi hospitali yetu imetukumbuka kwa kutuletea madaktari bingwa na kutuondolea gharama za kulipia ili kuonana nao, tuna imani kuwa changamoto zetu za afya zinaenda kupata tiba tukiwa hapahapa mkoani kwetu bila ya kusafiri" ameeleza. Kambi ya Madaktari Bingwa inajumuisha utoaji wa huduma za afya na matibabu ya kibingwa ya Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo, Uzazi, Magonjwa ya Watoto, Magonjwa ya ndani, Mifupa, Ngozi, Kinywa na Meno na Upasuaji.





Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.