Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Lindi Ndg. Mwinjuma Mkungu ameeleza kuwa Maonyesho ya nanenane yanatumika kama Jukwaa la kujifunza teknolojia bora za kuongeza uzalishaji katika zekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Akizungumza mbele ya viongozi wa serikali, wakulima, wadau wa maendeleo, wanafunzi na wananchi mbalimbali, Mkungu amepongeza juhudi za serikali zenye lengo la kuinua kipato cha mkulima na kuboresha maisha yake kwa kutoa pembejeo za kilimo bure kwa zao la korosho ambalo ndio zao kuu la biashara kwa wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
"Jumla ya Bilioni 305.9 zilitolewa na serikali ili kufanikisha zoezi la ugawaji wa pembejeo za kilimo bure kwa wakulima wa korosho ambapo 70 % ya wanufaika wa pembejeo hizo ni wakulima wa Mikoa ya Lindi na Mtwara ambao walipata sulphur pamoja na dawa za viuwatilifu vya kuulia wadudu" ameeleza
Aidha, amewapongeza wataalamu wa Halmashauri za Mikoa kwa jitihida zao za kutoa elimu ya kilimo bora, kusambaza pembejeo, na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa kwa wakulima vijijini hivyo kuleta ongezeko la tija katika kilimo, uboreshaji wa matumizi ya teknolojia na uanzishwaji wa viwanda vinavyochakata mazao ya wakulima.
"Juhudi mnazozifanya kwa kushirikiana na wakulima, taasisi za utafiti, sekta binafsi na wadau wengine ni za kupongezwa. Mmekuwa chachu ya mabadiliko ya kweli katika kilimo cha Kanda ya Kusini,” aliongeza.
Maonesho hayo yamehudhuriwa na washiriki kutoka taasisi mbalimbali za utafiti wa kilimo, vikundi vya wakulima, sekta binafsi, halmashauri na wanafunzi, ambapo wanatumia jukwaa hilo kuonyesha ubunifu, mafanikio, bidhaa na teknolojia mpya zenye uwezo wa kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini yataendelea hadi tarehe 8 Agosti 2025, yakitoa fursa kwa wananchi na wadau wa kilimo kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujionea mafanikio ya sekta ya kilimo kwa vitendo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.