Mhe. Mwakyembe: Hongereni wanalindi
Wananchi wa mkoa wa Lindi wamepongezwa kwa kutunza na kuhifandhi mila, desturi na utamaduni wao.
Pongezi hizi zimetolewa na Mhe. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alipokuwa akifungua tamasha la utamaduni wa watu wa Lindi kwa niaba ya Mhe. Samia Suluh Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani lililofanyika katika kijiji cha makumbusho mkoani Dar es Salaam.
Mhe. Mwakyembe alisema kuwa wanalindi kupitia tamasha hili la utamaduni wamefanikiwa kuonyesha mambo mbalimbali ya kiutamaduni. Pamoja na pongezi hizo, amewasihi wanalindi kuhakikisha wanaendelea kuzitunza tamaduni hizi kwa kuvirithisha vizazi vya sasa na vijavyo ili zisipotee.
“Wanalindi sasa inatakiwa mjipange kuhakikisha mnazitumia shughuli hizi za kiutamaduni kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla kwani hii inaweza kuwa ni fursa hata kwa watalii kuja kuona shughuli na kazi za kitamaduni zinazofanyika”, alisema Mhe. Mwakyembe.
“Serikali itaendelea kutunza, kulinda na kuhifadhi tamaduni za watanzania lakini hata wananchi wanao wajibu wa kuhakikisha tamaduni zetu zinatunzwa na kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo” alieongeza Mhe. Mwakyembe.
Aidha, ameupongeza uongozi wa Mkoa, ukiongozwa na Mhe. Godfrey Zambi, Mkuu wa Mkoa kwa dhamira njema ya kufanya tamasha la utamaduni na uendelezaji michezo. Pia ameipongeza wilaya ya Ruangwa kwa kujenga uwanja wa mpira wa miguu “Majaliwa Stadium” uliopo wilayani humo. Ujenzi wa uwanja huu ni fundisho kubwa hata kwa timu zetu ambazo zimekuwa zikicheza ligi kuu kwa miaka mingi lakini mpaka sasa hazijajenga kiwanja.
Kabla ya kumkaribisha waziri, Mhe. Zambi alisema kuwa tamasha lina wawakilishi kutoka katika kila halmashauri ambao wataonyesha shughuli mbalimbali za kitamaduni (zikiwemo ngoma, zana za asili, vyakula nk.) zilivyo katika maeneo yao.
Pia alitoa taarifa fupi ya hali ya maendeleo katika mkoa iliyoainisha vivutio vya kihistoria katika sekta ya utalii ambavyo unaweza kuvipata ukitembelea tovuti ya mkoa http://www.lindi.go.tz/economic-activity/utalii
Mhe. Zambi amemuhakikishia waziri kuwa mkoa umejipanga kuhakikisha kupitia tamasha hili watanzania wanapata fursa ya kuuelewa vizuri mkoa wa Lindi kwa kuanzia kwenye tamaduni zake. Aidha, alitumia fursa hii kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika mkoa wa Lindi kwani mkoa huo unazo fursa nyingi za kiuchumi. Pia aliwahakikishia wawekezeji kuwa viongozi na wananchi wapo tayari kutoa ushirikiano kwa yeyote yule atakayekuwa tayari kwenda kuwekeza.
Naye mwenyeji wa tamasha hili, Ndg. Mpanda alisema kuwa matamasha kama haya yanatoa fursa kwa watanzania kuweza kujifunza tamaduni za maeneo mengine na hivyo kuzidi kuimarisha mshikamano wetu. Pia amewaomba watanzania hasa wanaoishi Dar es Salaam kufika kwa wingi kujione mambo mbalimbali ya tamaduni za watu wa Lindi.
Mkurugenzi mkuu wa makumbusho ya taifa, Prof. Audax Mabulla amesema kuwa tamasha hili ni la 27 kufanyika katika kijiji cha makumbusho. Lakini kwa kuwa sasa kijiji cha makumbusho kinajengwa kwa kufuata ramani ya Tanzania, mkoa wa Lindi ndio umekuwa wa kwanza kujenga nyumba kwa kuzingatia hilo. Pia amewapongeza wanalindi kwa kufika kwa wingi na kuonyesha shughuli mbalimbali za kitamaduni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.