MHE. TELACK ASISITIZA UZALISHAJI WA KOROSHO ZENYE UBORA
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amefungua rasmi mnada wa korosho msimu wa 2025, katika chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao kinachosimamia wilaya za Lindi, Kilwa pamoja na halmashauri ya Mtama.
Mnada wa kwanza kwa msimu huu katika Mkoa wa Lindi umefanyika Oktoba 9, 2025 kwa kutoa matumaini makubwa kwa wakulima wa zao hilo la biashara mkoani hapa, huku Mhe. Telack akiwasisitiza wasimamizi wa Amcos na wasimamizi wa maghala kuepuka kupokea korosho chafu na kuhimiza uzalishaji wa korosho safi kwa kuzingatia ubora sahihi unaotakiwa katika ushindani kwenye soko la kimataifa, ambapo Tanzania imeendelea kuwa bora katika soko la kimataifa katika uzalishaji wa Korosho.
“Msipokee korosho chafu msipokee korosho ambayo haijapimwa unyevu na zile korosho zinazokuja hazijakauka vizuri hakikisheni wakulima mnawaelekeza vizuri wazianike zifikie kile kiwango kinachohitajika, napenda kusisitiza kwamba serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayejaribu kuhujumu korosho za mkulima, tunataka mkulima aliyeleta korosho zake amezichambua vizuri, amezikausha vizuri zibaki kama zilivyo na ziingie sokoni kama zilivyo ili apate bei kulingana na kazi aliyoifanya” amesisitiza Mhe. Telack.
Katika mnada huo uliofanyika chini ya usimamizi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), wakulima wameuza korosho ghafi kwa bei ya juu ya shilingi 2,460 na bei ya chini ya shilingi 2,310 kwa kilo ambapo zaidi ya tani 5,105 kilo 175 zimeuzwa katika mnada huo.







Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.