Mhe. Zambi: Viongozi na watendaji fanyeni kazi
Viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali za serikali katika mkoa wa Lindi watakiwa kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa kuhakikisha wanatatua kero za wananchi.
Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi katika kikao kazi alichokiitisha ambacho kiliwahusisha Wakuu wa Wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wakurugenzi wa Halmashauri, Viongozi wa Taasisi mbalimbali katika mkoa, wakuu wa idara na vitengo katika mkoa na halmashauri pamoja na wataalam wengine.
Mhe. Zambi amesema katika mkoa kuna baadhi ya watumishi ambao bado wanafanya kazi kwa mazoea kitu ambacho kinasababisha huduma zinazotolewa kwenye maeneo husika kuwa mbovu na hatimaye kusababisha wananchi kulalamika.
“Ni lazima kila kiongozi ahakikishe anawasimamia ipasavyo watumishi walio ndani ya taasisi yake au ndani ya eneo lake ili wafanye kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao”, alisema Mhe. Zambi.
“Viongozi na watumishi wote kwa ujumla ni lazima muelewe mnyororo wa ukubwa kazini kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na hata katika Taasisi zenu na kuhakikisha mnayafanyia kazi maelekezo/maagizo na ushauri utakaokuwa umetolewa na viongozi walio juu yenu”, aliongeza Mhe. Zambi.
Aidha, Mhe. Zambi aliwataka Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanazisimamia wilaya zao ili kuhakikisha wilaya zinasonga mbele kimaendeleo. Pia aliwataka waelewe na kufuatilia kwa karibu shughuli zote zinazofanywa na taasisi mbalimbali zilizopo katika wilaya zao.
Vilevile viongozi na watendaji wametakiwa kutoa huduma kwa kufuata mikataba kwa huduma ya taasisi huku taasisi ambazo bado hazina mikataba hiyo zikiagizwa kutengeneza. Taasisi zote zimeagizwa kuwasilisha mikataba hii kwa Mkuu wa MKoa mwezi Decemba, 2018.
Katika kikao hicho Mhe. Zambi alizungumza mambo mbalimbali ya kisekta mfano elimu, afya, kilimo, ugavi na mahakama, ambapo pia alitoa maelekezo mbalimbali huku kubwa akiwataka viongozi na watendaji kufanya kazi kwa weledi na kuacha kukaa maofisini badala yake kwenda kwa wananchi kutatua kero walizonazo.
Viongozi na watendaji kutoka taasis mbalimbali wakisikiliza maelekezo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.