Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe: Victoria Mwanziva kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amewapongeza wataalamu wa afya Mkoa wa Lindi kutoka katika Halmashauri zote sita kwa jitihada za kuhakikisha vifo vya mama na watoto wachanga vinapungua.
Mhe. Mwanziva ameyasema hayo katika kikao cha kujadili vifo vya wamama vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga hususan walio chini ya siku 28 kilichofanyika katima ukumbi wa mikutano, Shule ya Sekondari Nyanyao ambapo ameeleza kuwa katika Mkoa wa Lindi vifo vya mama vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka vifo 38 mwaka 2023 hadi kufikia vifo 27 mwaka 2024 lakini pia vifo vya watoto wachanga chini ya siku 28 vimepungua kutoka 272 mwaka 2023 hadi kufikia vifo 242 mwaka 2024.
Aidha, Mhe. Mwanziva amewasisitiza wataalamu kutilia mkazo zaidi udhibiti wa vifo vya watoto wachanga kwa kusimamia utekelezaji wa viashiria vya mama na mtoto pamoja na kutoa huduma za afya kwa kuzingatia kanuni, maadili na miiko ili kufikia lengo la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Aidha DC Mwanziva amempongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKT. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya afya uliosaidia mafanikio hayo ya kupunguza idadi ya vifo ndani ya mwaka mmoja, jitihada hizo ni pamoja na ujenzi wa hospitali ya Mkoa, ujenzi wa hospitali mpya za Halmashauri ikiwemo hospitali ya Wilaya ya Mtama iliyopo Kiwalala pamoja na marekebisho mbalimbali katika vituo vya afya na zahanati.
Kikao hiko kimewakutanisha wadau mbalimbali wanaofanya kazi za kuratibu shughuli za afya ya mama na mtoto ikiwemo Timu za usimamizi wa afya ngazi za wilaya na Mkoa (CHMTs na RHMT) za Mkoa wa Lindi, Timu ya Madaktari wasio na Mipaka (MSF), MSD, Marie Stoppes na wengineo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.