MNADA WA PILI RUNALI; KOROSHO ZAUZWA KWA BEI YA JUU TSH 2730 NA YA CHINI TSH 2590.
Mnada wa pili wa korosho wa Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI umefanyika Novemba 16, 2025 katika ghala la Lipande Wilayani Ruangwa ambapo katika mnada huo jumla ya tani 18,601 za korosho zimeuzwa kupitia mnada ulioendeshwa kwa mfumo wa TMX.
Wakulima wamekubali kuuza korosho zao kwa bei ya juu Tsh 2,730 kwa kilo huku bei ya chini ikiwa ni Tsh 2,590 kwa kilo baada ya ushindani mzuri kutoka kwa wanunuzi na kuashiria muendelezo wa matumaini katika msimu wa mauzo ya korosho.
Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Hassan Ngoma amepongeza uendeshaji wa mnada huo na kuwataka wakulima kuendelea kuboresha uzalishaji na ubora wa zao la korosho ili kuongeza thamani na ushindani kwenye soko la ndani na nje ya nchi na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uboreshaji wa sekta ya kilimo ili kumpa tija mkulima katika uzalishaji na kuboresha hali ya maisha.
Aidha, amewataka viongozi wa vyama vya Ushirika na Amcos kufuata sheria, taratibu na kanuni za Ushirika ili kumuwezesha mkulima kupata stahiki zake na kuwasisitiza wakulima kuandaa vyema mazao yao kwa kuzingatia vigezo na viwango vya ubora vinavyohitajika sokoi ili kuzidi kupata bei nzuri za mazao yao.
Mwenyekiti wa RUNALI, Bwn. Odas Mpunga amewasisitiza wakulima kuhakikisha korosho zao zinakaushwa vizuri ili kuendelea kupata bei nzuri sokoni na kuwakumbusha kuwa upelekaji wa korosho chafu na zenye unyevu sokoni hupelekea
kudororesha bei na kuharibu sifa za mazao yanayopatikana katika ukanda huu sokoni.




Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.