Mkoa wa Lindi Leo Jumanne tarehe 11 Aprili 2023 umeupokea mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Mtwara, ambapo makabidhiano yamefanyika katika kiwanja cha mpira cha Nyangao, Halmashauri ya Mtama.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack amekabidhiwa Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Abbas Ahmed Abbas. Sambamba na hilo Mhe. Telack amewapokea wakimbiza mwenge 6 wakiongozwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Ndg. Abdalla Shaib Kaim.
Akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack amesema kuwa Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Lindi utakimbizwa kwenye njia ya kilomita 1050.1 na kuipitia jumla ya Miradi 61 ya maendeleo yenye thamani ya Bilioni 51.5. Kati ya Miradi hiyo 61 , Mwenge wa Uhuru utaweka nawe ya msingi kwenye miradi 15, utazindua Miradi 10, kutembelea na kuona Miradi 36.
Mhe. Telack amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchangia asilimia 98 ya fedha za kutekeleza Miradi yote 61 itakayopitiwa na Mwenge wa Uhuru. Huku asilimia 12 ya fedha zilizobaki zimetoka kwa wadau wa maendeleo, Halmashauri pamoja na nguvu ya wananchi.
Akimkaribisha Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Mhe. Telack ameongeza kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri zote 6 za Mkoa wa Lindi ambapo Halmashauri ya Mtama itakuwa ya kwanza.
Kwa upande wake, Kiongozi wa mbio za Mwenge, Ndg. Abdalla Shaib Kaim amesisitiza uwepo wa Nyaraka zote muhimu katika maeneo ya miradi sambamba na wataalam wanaohusika na Miradi hiyo.
Mkoa wa Lindi unakuwa Mkoa wa Pili kuukimbiza Mwenge wa Uhuru baada ya Mkoa wa Mtwara ambapo zilifanyika sherehe za uzinduzi kitaifa tarehe 01 Aprili 2023.
Aidha, Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru Kwa mwaka 2023 inasema " Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji Kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.