Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amebainisha kuwa Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza kutolewa kwa leseni ya uchimbaji madini ya nikeli kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kwa Wachimbaji wadogo waliokuwepo katika eneo la vilima vya Ntaka- Nachingwea, Mkoani Lindi.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 08 Julai, 2025 katika mkutano wa hadhara wa wananchi na wachimbaji katika Kijiji cha Nditi punde tu baada ya kufanya ziara ya kutembelea maeneo na migodi ya wachimbaji wadogo chini ya Umoja wa Vikundi vya Wachimbaji Madini (UVIWAMA).
" Rais Dkt. Samia Hassan amesikia kilio chenu cha muda mrefu cha kutaka kupewa maeneo ya uchimbaji katika Leseni inayomilikiwa na Serikali. Na ndiyo maana nimefika hapa kuja kuwaletea habari njema wachimbaji wadogo kwamba, hatutawaondoa katika eneo mnalochimba na tunakwenda kuwarasimisha," amesema.
"Pamoja na kupewa eneo la uchimbaji, amewasihi wachimbaji wadogo kufuata taratibu kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura ya 123 ambayo inaelekeza mwenye haki madini kuhakikisha anapata ridhaa ya mwenye haki ardhi kabla hajaanza uchimbaji, ili kuepusha migogoro katika shughuli zao za uchimbaji.
Rais Dkt. Samia ameelekeza eneo la leseni hiyo lenye ukubwa wa Kilometa za Mraba 45 ipewe (STAMICO) kwa ajili ya kuanza uchimbaji mkubwa wa nikeli ndani ya miezi 18 ijayo kama Sheria ya Madini inavyoelekeza.
"Kwa kuwa kwenye Leseni hii Serikali ililipa zaidi ya shilingi bilioni 243 kama fidia, ni lazima sasa STAMICO na wachimbaji wadogo wafanye uchimbaji wenye tija ili kurejesha fedha hizo katika mfuko mkuu wa Serikali," amesema Mavunde.
@wizara_ya_madini_tanzania
@ortamisemi
@maelezonews
@msemajimkuuwaserikali
@gersonmsigwa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.