Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary leo amepokea rasmi vifaa vya uchunguzi na matibabu ya macho vyenye thamani ya shilingi milioni 56, vilivyotolewa na Shirika la Kimataifa la Sightsavers kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi – Sokoine.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika hospitali hiyo, RAS. Zuwena amesema kuwa msaada huo ni kielelezo cha ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuboresha huduma za afya, hususan huduma za macho kwa wananchi.
Licha ya pongezi hizo, RAS ametoa rai kwa watoa huduma za afya katika hospitali ya sokoine kuhakikisha vifaa hivyo vinaleta tija kwa wananchi kwa kuhakikisha uboreshaji wa huduma zinazotolewa kwa wananchi. Vilevile, ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma za macho katika hospitali hii na kuwahakikisha kupata huduma stahiki wanayoitarajia.
Kwa upande wake, Meneja mradi wa Sightsavers amesema kuwa vifaa hivyo ni sehemu ya mkakati wa shirika hilo kusaidia upatikanaji wa huduma jumuishi na rafiki kwa watu wote.
Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi umeishukuru Sightsavers kupitia Ndugu. Peter Kivungi ameeleza kuwa vifaa hivyo vitaongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma bora za macho, ikiwemo upimaji wa macho, uchunguzi wa kina, na tiba stahiki kwa wagonjwa.
Katibu Tawala Msaidizi Afya, Dkt. Kheri Kagya ameeleza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wadau wote wanaojitokeza kusaidia sekta ya afya, huku ikisisitiza matumizi sahihi na uendelevu wa vifaa hivyo kwa maslahi ya wananchi wa Lindi na Tanzania kwa ujumla.
Vifaa vilivyopokelewa leo ni pamoja na mashine ya B-scan ya macho (1), hadubini ya upasuaji (1), seti ya vifaa vya upasuaji wa mtoto wa jicho (3), lenzi ya 90D kwa uchunguzi wa retina (1), seti ya lenzi za majaribio (1), fremu ya majaribio kwa watu wazima (1) na fremu ya majaribio kwa watoto (1).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.