Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Jiri amewasisitiza maafisa biashara wa halmashauri za Mkoa wa Lindi kutumia mfumo wa Tausi ili kuboresha ukusanyaji wa mapato ya halmashauri kupitia kodi za leseni, kodi za majengo,kodi za mabanda, kodi za mabango na vibali vya ujenzi.
Katibu Tawala amesisitiza hayo wakati wa kufunga mafunzo ya siku tano yenye lengo la kutoa uelewa juu ya Maboresho ya Mfumo wa Tausi na Muse na utekelezaji wake katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa vibali kwa Maafisa biashara, Maafisa Ardhi na Wahandisi wa Halmashauri.
Akizungumza katika mafunzo hayo, katibu tawala ameeleza kuwa awali Halmashauri zimekua zikipata hasara nyingi na hoja zisizo za ulazima hivyo kupelekea kukosa makusanyo katika kodi ikiwemo kodi za mabanda,mabango, kodi za upandikishaji wa mabanda ya biashara, leseni za biashara, na vibali vya ujenzi na lazima kutokana na kukosa ujuzi na uelewa wa kutosha ya matumizi ya mfumo wa Tausi katika maeneo hayo.
"Mmejifunza kuzingatia na kufuata sheria, taratibu na miongozo zinazosimamia usimamizi,ukusanyaji wa mapato, uhasibu na uhandisi ili kuepuka hoja za kiukaguzi na tunaamini maarifa haya yatachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha utendaji wa kazi na ukusanyaji wa mapato katika halmashauri zenu. Ni matarajio yetu kuwa mtaenda kufanya kazi kwa kuzingatia na kulingana na matarajio ya taasisi" Ameeleza.
Frank Kihunga, Mhandisi wa Halmashauri ya Ruangwa amesema mafunzo haya yamewapa mwanga wa matumizi ya vipengele vya mfumo wa Tausi ambavyo mwanzoni hawakua wakivitumia kutokana na kutokuwa na uelewa wa namna ya kuvifanyia kazi.
"Mafunzo haya ya maboresho ya mfumo wa Tausi yametupa uelewa wa matumizi ya vipengele ambavyo awali havikua vikitumika ikiwemo utoaji wa vibali vya ujenzi hivyo kuboresha mfumo mzima wa ukusanyaji wa mapato" ameeleza.
Naye, Bi. Ntuli Mwakyonde, Afisa Ardhi Halmashauri ya Kilwa ameeleza kuwa kupitia mafunzo haya wamejifunza namna ya uuzaji wa viwanja kupitia mfumo wa Tausi na namna ambavyo umerahisisha utendaji wa kazi.
"Kupitia mfumo huu mtu yoyote anaweza kupata huduma ya kuchagua na kununua kiwanja chake bila kuja ofisini hivyo kupunguza msongamano wa wananchi katika ofisi pamoja na urasimu" ameongeza Bi. Ntuli.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.