RAS LINDIi: ELIMU YA UHIFADHI NI MUHIMU KWA MAENDELEO ENDELEVU.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi ameongoza maadhimisho ya Siku ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini, yaliyofanyika katika viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, RAS alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuielimisha jamii juu ya uhifadhi wa maliasili na mazingira, akibainisha changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo zikiwemo uvamizi wa mifugo kwenye hifadhi, migogoro kati ya wafugaji, wakulima na wahifadhi pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Ameendelea kwa kusema kuwa elimu endelevu kwa wananchi ni msingi muhimu wa kuhakikisha rasilimali hizi zinawanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo. Aidha, alitoa wito kwa taasisi zote za uhifadhi kuongeza ubunifu katika utoaji wa elimu kwa jamii kwa njia shirikishi na rafiki.
Katika tukio hilo, RAS alipata fursa ya kujionea wanyamapori waliopo katika mabanda ya maonesho, kujifunza kuhusu shughuli za uhifadhi na kushiriki katika mlo wa pamoja uliokuwa na nyama ya wanyamapori waliovunwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa Kamanda wa TFS, taasisi hiyo inasimamia jumla ya misitu 54 katika Ukanda wa Kusini, ikiwa ni pamoja na maeneo ya pwani ya mikoko na bara, pamoja na mazalia 9 ya nyuki. Kwa upande wa TAWA, jumla ya maeneo 7 ya hifadhi yanayofikia km² 16,654 yanasimamiwa, ikiwemo Pori la Akiba la Selous.
Takwimu zinaonesha kuwa watalii zaidi ya 15,000 walitembelea Ukanda wa Kusini mwaka 2024/2025, huku Wilaya ya Kilwa ikipokea meli 8 za kitalii kutoka nje ya nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.