RC LINDI AWAKABIDHI JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI MKOA WA LINDI MAGARI YA KISASA.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, Leo Oktoba 24, 2025, amekabidhi vitendea kazi kwa Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Lindi, wakati wa zoezi la utayari uliohusisha na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Lindi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha utendaji wa kazi na kukabiliana na changamoto wakati wakati wa utekelezaji wa majukumu yao. Vitendea kazi vilivyokabidhiwa ni Magari ya ufuatiliaji na usimamizi pamoja na gari la wagonjwa la kisasa, Coman Car, Mtambo (Motor) Unaobeba Litre 5,000 za maji na povu la kemikali (chemical foam) ujazo wa lita 400 pamoja na gari dogo la ukaguzi. Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Telack amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo vyombo vya Ulinzi na Usalama ili viweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Haya ni matokeo ya dhamira ya Serikali kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinakuwa na vitendea kazi vya kisasa. Ni jukumu letu sasa kuvithamini na kuvitumia kwa uadilifu katika kulinda usalama wa wananchi,” alisema Mhe. Telack.
Aidha, aliwataka maafisa wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuimarika hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
“Tuendelee kudumisha amani na kuhakikisha wananchi wanatekeleza haki zao za kupiga kura bila wasiwasi. Vyombo vyetu viwe mstari wa mbele katika kuilinda amani hii,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mrakibu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Lindi, Joseph Mwasabeja ameishukuru Serikali kwa kuleta vifaa hivyo ambavyo vitasaidia kwa kiwango kikubwa kutatua changamoto zilizokuwa zinajitokea wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
“Kupata vifaa hivi ni hatua kubwa kwetu. Vitatusaidia kuongeza kasi na ufanisi katika kukabiliana na matukio ya dharura na majanga, Kwa kiwango kikubwa sasa tumepata vifaa vingi vitaenda kutatua changamoto tulizokuwa tunakutana nazo” amesema Mwasabeja.












Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.