RC MTWARA
- Wataalamu watakiwa kutoa elimu stahiki kwa wananchi ili kuleta tija.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala, leo tarehe 01 Agosti 2025, amezindua rasmi Maonesho ya 12 ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kwa Kanda ya Kusini yanayofanyika katika Viwanja vya Ngongo, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, mkoani Lindi.
Akihutubia wakati wa ufunguzi, Kanali. Sawala amewataka wataalamu wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kuhakikisha wanatoa elimu stahiki na ya kisasa kwa wananchi, ili kuongeza maarifa na ubunifu katika shughuli zao za uzalishaji.
"Maendeleo ya sekta hizi yanategemea kwa kiasi kikubwa uhamasishaji wa matumizi ya teknolojia mpya, pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya wataalamu na jamii" ameongeza.
Pia, ameeleza kuwa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini ni jukwaa muhimu la mafunzo, maonesho ya teknolojia, ubunifu na fursa za kibiashara. Maonesho haya hufanyika kila mwaka yakijumuisha mikoa ya Lindi na Mtwara hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuhakikisha wanatumia maonyesho hayo kujifunza mambo mapya yahusuyo kilimo ili waweze kuongeza uzalishaji.
Aidha, Kanali Sawala amewakumbusha wananchi kujiandaa na kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika ifikapo Oktoba, 2025 ili wapate nafasi ya kuchagua viongozi wanaowafaa na watakaochochea upatikanaji wa maendeleo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Kaulimbiu ya maonesho ya mwaka 2025 ni:“Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.