Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Kenan Sawala, amesema kuwa Maonesho ya Madini ya Lindi Mining Expo 2025 ni nguzo muhimu ya maendeleo kwa Ukanda wa Kusini, kutokana na mchango wake katika kuongeza uelewa, kuhamasisha ushiriki wa wadau, na kuvutia wawekezaji katika sekta ya madini.
Kauli hiyo ameitoa leo, tarehe 12 Juni 2025, wakati akifungua mafunzo ya kuongeza uelewa na ujuzi katika sekta ya madini kwa wadau wa madini mkoani Lindi, wakiwemo wachimbaji wadogo, ambao ni kundi mhimu katika mafunzo hayo.
Aidha, Kanali Sawala amesema kuwa Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa mikubwa nchini yenye uzalishaji mkubwa wa madini, hivyo kupitia maonesho haya wananchi wa Lindi, mikoa ya jirani, na hata nje ya nchi wamepata fursa ya kujifunza, kujionea utajiri uliopo, na kuwekeza katika rasilimali hizo kwa manufaa ya kiuchumi.
“Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa mikubwa kwenye nchi yetu inayozalisha madini kwa wingi, maonesho haya yamekuwa na faida kubwa kwa kuongeza uelewa kwa wanalindi, mikoa ya jirani, nchi kwa ujumla na hata nje ya nchi yetu, kwa kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza Lindi na kujionea utajiri mkubwa unaopatikana. Hii inadhihirisha kuwa Lindi Mining Expo 2025 ni fursa kubwa kwa Ukanda wa Kusini,” amesea Kanali Sawala.
Vilevile, amesisitiza kuwa mashirikiano kati ya Mkoa wa Lindi na Mtwara yamekuwa na tija, kwani maonesho hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali kutoka pande zote mbili, ikiwemo wachimbaji, wawekezaji na wataalamu wa sekta ya madini.
Kwa upande mwingine, amewahimiza wachimbaji wadogo kutumia maarifa watakayoyapata katika mafunzo hayo kuongeza tija na ufanisi, ili sekta ya madini iendelee kuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa mikoa ya Kusini na taifa kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.