Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, ameongoza mbio za ridhaa za kilometa 5 zilizofanyika leo, Juni 12, 2025, wilayani Ruangwa, kama sehemu ya shamrashamra za maonesho ya madini na fursa za uwekezaji maarufu kama Lindi Mining Expo 2025.
Tukio hilo limehudhuriwa na wananchi kwa wingi, likiwavutia wakazi wa Ruangwa pamoja na wageni kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Mkoa wa Lindi. Mbio hizo zimechangia kuhamasisha ushiriki wa jamii katika shughuli za kimaendeleo, huku pia zikiashiria uzinduzi rasmi wa wiki ya maonesho hayo muhimu.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, ameeleza kuwa tukio hilo limeonesha mshikamano mkubwa wa jamii na linaakisi mwamko chanya wa wananchi kushiriki katika maendeleo ya Mkoa kupitia sekta ya madini.
“Mbio hizi ni mwanzo mzuri wa kuhamasisha ushiriki wa jamii katika maonesho haya makubwa ya madini, tunahitaji mshikamano wa wananchi, wawekezaji na wadau wote ili kuhakikisha rasilimali zetu zinawanufaisha watu wa Lindi na Taifa kwa ujumla.” Amesema Mhe. Telack
Kwa mujibu wa waandaaji wa maonesho hayo, mbio hizo zililenga kuunganisha jamii, sekta binafsi, na Serikali katika kujenga mshikamano na uelewa juu ya fursa za kiuchumi kupitia sekta ya madini. Washiriki wameonesha ari kubwa, huku baadhi yao wakieleza kufurahishwa na namna tukio hilo lilivyowapa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika maandalizi ya maonesho hayo.
Lindi Mining Expo 2025 inatarajiwa kufanyika kwa siku nne kuanzia Juni 11 hadi 14, ikiwa ni jukwaa mahsusi la kuonyesha raslimali za madini, kuhamasisha uwekezaji, na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.