Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omari, ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kupata Hati Safi kwa miaka sita mfululizo katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ametoa pongezi hizo leo tarehe 17 Juni, 2025 katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Ruangwa kwa ajili ya kuchambua na kujadili taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha 2023/2024.
Kikao hicho kimehusisha Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri hiyo, Wakuu wa Idara na Vitengo (CMT), Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Wakaguzi kutoka Ofisi ya CAG Mkoa wa Lindi, Katibu wa Waziri Mkuu, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Katibu Tawala wa Wilaya pamoja na wajumbe wa Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi.
Aidha, akiwasilisha salamu za Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack, Bi. Zuwena amesema kupata Hati Safi kwa miaka mitano mfululizo ni ishara ya utendaji bora, uwajibikaji wa hali ya juu na usimamizi mzuri wa rasilimali za umma.
“Niwapongeze kwa dhati kwa kupata Hati Safi kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo, hii siyo kazi rahisi bali ni matokeo ya mshikamano, uadilifu na kujituma kwa viongozi wa kisiasa na wataalamu wa Halmashauri ya Ruangwa,” amesema Bi. Omari
Vile vile, ameongeza kuwa ufanisi huo unapaswa kuwa mfano kwa Halmashauri nyingine ndani ya Mkoa na kuwataka viongozi waendelee kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ili kuimarisha zaidi mifumo ya kifedha na kiutawala.
Sambamba na hayo, Bi. Zuwena ameagiza hoja zote zinazoweza kufutwa zifanyiwe kazi na ili zifutwe mara moja maana zipo ndani ya uwezo wa Halmashauri.
Baraza hilo maalumu ni sehemu ya utekelezaji wa sheria ambapo Madiwani hukutana kuchambua taarifa ya ukaguzi wa CAG kwa lengo la kuweka mikakati ya maboresho na kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.