Lindi, Agosti 8, 2025 — Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, amesema Serikali haitaendelea kuruhusu usafirishaji wa mazao ghafi nje ya nchi, kwani hatua hiyo inapoteza fursa nyingi za ajira kwa vijana na kudhoofisha uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika hafla ya ufungaji wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini kwenye Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi, Dkt. Jafo amepongeza juhudi za Vyama vya Ushirika vinavyoongeza thamani ya mazao, hususan kwa kuanzisha viwanda vya ubanguaji wa korosho, akisisitiza kuwa hiyo ndiyo njia sahihi ya kulinda uchumi na kuongeza mapato kwa wakulima.
“Badala ya kuuza korosho ghafi, tunapaswa kuziongeza thamani hapa nchini ili vijana wapate ajira na wakulima wafaidike zaidi,” amesema Dkt. Jafo.
Waziri huyo amewataka wananchi wa Lindi na Mtwara kutumia maarifa na teknolojia walizojifunza kwenye maonesho hayo kwa vitendo, ili kuboresha uzalishaji na kuinua kipato chao, hatua itakayochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha, ameipongeza sekta ya fedha, hususan mabenki, kwa kutoa elimu na mikopo yenye riba nafuu isiyozidi asilimia 10 kwa wakulima, wavuvi na wafugaji. Pia, amewataka wataalamu wa Serikali kuwa chachu ya maendeleo badala ya kuwa kikwazo kwa wajasiriamali na wakulima.
Kwa upande mwingine, Dkt. Jafo amezitaka taasisi za SIDO na TBS katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuhakikisha zinawasaidia wajasiriamali kukua kiuchumi kupitia kilimo, uvuvi na biashara ndogondogo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.