Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga, kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amezindua awamu ya tatu ya mradi wa Timiza Malengo 2024-2026 unaotarajiwa kutekelezwa katika Mikoa 10 na Halmashauri 36 nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mhe. Ummy amesema kuwa mradi wa Timiza Malengo unalenga kupunguza maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa vijana balehe wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 24 walio mashuleni na nje ya mfumo wa elimu kwa kuwajengea uwezo wa kujikinga dhidi ya maambukizi na kuwawezesha kiuchumi katika Mikoa ya Singida, Lindi, Morogoro, Njombe, Dodoma, Tabora, Tanga, Ruvuma, Geita na Mara.
Aidha, Mhe. Ummy ameeleza kuwa serikali inaendelea na mipango ya kisera na kimuundo kuhakikisha hadi ufikapo 2030 Tanzania iwe imefanikiwa kufikia 03 katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya, kuzuia vifo vitokanavyo na VVU/UKIMWI pamoja na unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na maambukizi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Catherine Joachim, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza mradi huo, akibainisha kuwa itawafikia vijana balehe walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU na kusaidia kupunguza kasi ya maambukizi nchini.
Pia, Dkt. Catherine ameeleza kuwa mradi utasaidia kufikia malengo ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika mapambano dhidi ya UKIMWI ifikapo 2030, kuongeza wigo wa utekelezaji wa afua za kinga kwa vijana, kutunisha mfuko wa udhamini pamoja na kuboresha mifumo ya uratibu.
Aidha, mradi wa Timiza Malengo kwa awamu ya tatu umelenga kuwafikia na vijana balehe wa kiume na kuwapa mafunzo stadi, kuwaunganisha na taasisi za ufundi hususan VETA, pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo nafuu ikiwemo mikopo ya 10% inayoratibiwa na serikali kupitia wizara ya TAMISEMI.
Sambamba na uzinduzi wa mradi wa Timiza Malengo, Mhe. Ummy amezindua kampeni ya Tusonge na Samia Kutokomeza UKIMWI, ambayo inalenga kuhamasisha utekelezaji wa afua mbalimbali za kudhibiti VVU na UKIMWI nchini, kampeni hii inatarajiwa kuongeza mwamko wa jamii kuhusu hatua madhubuti za kujikinga na kusaidia katika kufanikisha lengo la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.