KAULI MBIU “Mbegu Zetu, Hazina Yetu, Urithi Wetu, Tuzitunze”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi Maalum, Mhe. George Mkuchika, ameongoza maadhimisho ya Maonesho ya Mbegu na Vyakula vya Asili Kanda ya Kusini yanayofanyika katika Viwanja vya Ngongo, Manispaa ya Lindi, ambapo amesisitiza umuhimu wa kurudi katika matumizi ya mbegu na vyakula vya asili kama njia ya kulinda afya na maisha ya jamii.
Amesema jamii nyingi zimehamia kwenye matumizi ya vyakula vya kisasa vilivyosindikwa kwa kemikali nyingi, hali inayochangia kuongezeka kwa magonjwa.
“Leo hata sisi watu wazima tumekumbwa na ugonjwa wa kupenda vyakula vya kisasa. Turejee kwenye vyakula vya asili kama walivyofanya mababu zetu ili tuishi maisha marefu na salama,” alisema Mhe. Mkuchika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SWISSAID Tanzania, Bi. Betty Malaki, amesema taasisi hiyo imeanza awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi kwa mwaka 2025 hadi 2028, ikilenga kuweka msukumo zaidi kwenye kilimo ekolojia, usawa wa kijinsia, na utunzaji wa mazingira kwa lengo la kuboresha ustawi wa kaya na kuimarisha uhuru wa chakula nchini. Alisema lengo ni kuwezesha jamii kuzalisha kwa njia endelevu, bila kuathiri mazingira wala afya.
Naye Dkt. John J. Tenga, Mtafiti Mkuu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), alieleza kuwa taasisi hiyo inashirikiana kwa karibu na wakulima kupitia tafiti shirikishi ili kuboresha mbegu za asili kwa manufaa ya mkulima. “Majibu tunayoyapata kutoka kwa wakulima tunayatumia kuboresha mbegu hizi ili kumpatia mkulima tija zaidi,” alisema Dkt. Tenga.
Katika kilele cha maadhimisho hayo, wakulima kutoka maeneo mbalimbali ya kanda ya kusini walibadilishana mbegu za asili, kama sehemu ya juhudi za kuzihifadhi na kuendeleza kilimo cha asili chenye tija. Tukio hilo lilifuatiwa na ushirikiano wa pamoja kwenye mlo wa asili ambapo washiriki walijumuika kufurahia vyakula vya kitamaduni ikiwemo matamba (ugali wa muhogo), uji wa njugumawe, mboga ya balaoa, pilau ya asili, upupu, ming’oko na chikandanga.
Maonesho haya yameonesha mshikamano wa wadau katika kuenzi urithi wa kilimo na lishe ya asili na kutoa dira ya maisha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.