Utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI kwa mwaka 2016/2017 wazinduliwa Mkoani Lindi.
Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Shaibu Ndemanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa amezindua zoezi la utafiti wa viashiria vya vvu/ukimwi kwa mkoa wa lindi katika Mkutano wa Wadau uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Zoezi hili litahusisha ukusanya taarifa zinazohusiana na maambukizo mapya ya VVU, kiwango cha VVU mwilini kwa watu wanaoishi na VVU na wastani wa maambukizo ya VVU kwa watu wa rika zote na wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4 T-cell count). Utafiti huu utahusisha wananchi wa rika zote katika kaya zilizochaguliwa.
Pia utafiti huu utaangazia kuwepo kwa Viashiria vya usugu wa dawa, kiwango cha maambukizo ya kaswende na homa ya ini (Hepatitis B na C) kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi. Pamoja na hayo utafiti huu utakusanya taarifa za upatikanaji na utumiaji wa huduma zitolewazo katika kudhibiti maambukizo ya VVU na UKIMWI na Viashiria vya tabia hatarishi zinazochangia maambukizo ya VVU.
Utafiti wa aina hii ni wa nne kufanyika hapa nchini, unaoangalia maswala ya afya ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2003/2004, wa pili ulifanyika 2007/2008 na Utafiti wa tatu ulifanyika 2011/2012.
Mhe. Ndemmanga alisema utafiti huu utaiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi zitakazosaidia katika kupanga mikakati sahihi ya kuendeleza mafanikio yanayoonekana katika mapambano dhidi ya UKIMWI ili kuokoa nguvu kazi ya taifa ambayo ni ya msingi katika kufanikisha jitihada za serikali yetu za kupambana na umaskini.
“Mtakubaliana nami kwamba, Sera na Mipango bora hutegemea sana upatikanaji wa takwimu sahihi na bora. Hivyo nitoe wito kwa wadau wote wa mkoa wetu kutoa ushirikiano wa Karibu kwa watafiti/Wadadisi ili kufanikisha zoezi hili muhimu kwa taifa letu, alisema Mhe. Ndemanga.
Aidha, amevisihi vyombo vyote vya habari, kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii ili kuzihimiza kaya zilizochaguliwa kutumia fursa hii adimu kujua afya zao bure bila malipo na kujiweka huru badala ya kuendelea kuishi kwa wasiwasi kwa tatizo ambalo hivi sasa linadhibitika kuliko ilivyokuwa siku za nyuma.
Mh. Ndemanga amewasihi wananchi wa Mkoa wa Lindi kuwa na mazoea ya kupima afya kwenye vituo vya afya ambavyo kwa sasa ni vingi ikilinganishwa na zamani, kupokea majibu ya vipimo na kujiunga katika huduma za tiba kwa wakati kwa kadiri itakavyoshauriwa na wataalamu wa afya.
Mkutano huu wa uzinduzi wa zoezi la utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi 2016 uliwashirikisha Makatibu Tawala wa Wilaya zote, Wawakilishi wa TACAIDS, Wawakilishi wa NBS, Wawakilishi wa ICAP, Viongozi wa Dini na Waandishi wa Habari pia ulihudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Ndugu Valentine Ndyano.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.