WADAU WA MAENDELEO YA JAMII LINDI WAKUTANA KUJADILI MPANGO MKAKATI WA KUPINGA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO.
Mkoa wa Lindi umefanya kikao na wadau mbalimbali wa Maendeleo ya Jamii wakiwemo wadau kutoka serikalini, asasi za kiraia na taasisi za dini kwa lengo la kupitia rasimu ya Mpango Mkakati wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2025/26- 2029/30).
Ndugu. Charles Kigahe, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Lindi ameeleza kuwa Rasimu hiyo imejikita katika kuimarisha ulinzi, ustawi na fursa kwa wanawake na watoto kwa kuelekeza nguvu kubwa katika kuboresha haki za binadamu, huduma muhimu za kijamii, uwezeshaji kiuchumi na kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
Katika majadiliano hayo, wadau walisisitiza umuhimu wa kuimarisha masuala ya haki za binadamu kwa kuhakikisha wanawake na watoto wanapata hifadhi, usawa na msaada pale wanapokumbana na vitendo vya ukatili kwa kuboresha huduma za ustawi wa jamii zikiwemo huduma za msaada wa kisheria, usaidizi wa kisaikolojia, ulinzi wa mtoto na mifumo rafiki ya utoaji taarifa za ukatili.
Aidha, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kupitia mafunzo, mitaji midogo, ajira na programu za kuinua uchumi wa kaya zinatarajiwa kupunguza utegemezi unaowafanya wanawake wengi kuwa katika hatari ya kunyanyaswa na kukosa uhuru wa maamuzi.
Wadau pia walijadili kwa kina changamoto ya mdondoko wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari unaochangiwa na mila na desturi zisizofaa kama Jando na Unyago hususan inapotekelezwa bila kuzingatia haki na ustawi wa watoto, pamoja na changamoto ya kukosekana kwa chakula shuleni ambayo husababisha wanafunzi wengi kukatisha masomo na kupendekeza mikakati madhubuti ya kuelimisha jamii, kuimarisha huduma shuleni na kuweka mifumo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha watoto wanasalia shuleni na kumaliza masomo.
Mpango mkakati huu unatarajiwa kuwa nyenzo muhimu katika kupunguza ukatili, kuimarisha ustawi wa wanawake na watoto, na kupandisha kiwango cha elimu katika Mkoa wa Lindi kwa miaka ijayo.





Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.