- "CHW, Nyumba kwa Nyumba, Hatuachi Mtu"
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Afya imekabidhi seti ya vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) 3,561 waliohitimu mafunzo ya kutoa huduma za afya ngazi jamii.
Katika hafla ya kukabidhi vyeti na vitendea kazi kwa wahitimu 222 wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, wakiwakilisha kundi la Wahudumu 3,561 wa awamu ya kwanza ya wahudumu waliohitimu mafunzo hayo katika mikoa 12, Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omary amewataka wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii WAJA kuzingatia miongozo, taratibu,maadili na tahadhari zote walizoelekezwa kipindi cha mafunzo wanapokwenda kutoa huduma katika jamii zao ili kufikia lengo la mpango wa serikali wa kuongeza nguvu kazi na kuwasogezea wananchi huduma za afya msingi na matibabu ya awali.
Aidha, Bi. Zuwena amesema Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya karibu zaidi na wananchi na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wamehitimu na wapo tayari kwa ajili ya kuanza kazi wakiwa na nyenzo zote muhimu kwa ajili ya kufanya kazi kwa ufanisi.
“Mpango huu ulizinduliwa mwaka 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango, hapo nyuma katika miaka 1970 tulikuwa na mpango huu pia lakini ulipitia changamoto za uratibu na awamu hii programu hii ya WAJA imeboreshwa zaidi ili kuleta tija zaidi katika kuimarisha huduma za kinga ndani ya jamii ili kufikia lengo la Huduma za Afya kwa wote ifikapo mwaka 2030,” amesema Bi. Zuwena.
Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Kheri Kagya amesema ni matarajio ya serikali kuwa uwepo wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii utasaidia utolewaji wa huduma za afya, Uzazi na mtoto, Lishe, Usafi wa mazingira na magonjwa ya mlipuko pamoja na kuwa kiunganishi muhimu baina ya jamii na vituo vya kutolea huduma za afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.