Watendaji wa Uchaguzi Ngazi ya Mkoa leo 17, Januari 2025 wamekula Kiapo cha Utii mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Lindi Mhe. Consolata P. Singano katika hafla ya Mafunzo kuhusu Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mst) Mbarouk S. Mbarouk,Makamu Mwenyekiti wa INEC amewasisitiza watendaji wa uchaguzi kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji kwa kuzingatia kuwa vinatarajiwa kuendelea kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini.
Mafunzo hayo yamehusisha namna ya ujazaji fomu pamoja na kutumia mfumo wa wapigakura yaani Voters Registration System - VRS ili kupata uelewa utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo huo na vifaa vingine pamoja na kuwajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi wa Kata ambao watatoa mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao watahusika kuandikisha Wapigakura vituoni.
Aidha, kwa kuzingatia kuwa matokeo bora ya zoezi la uandikishaji yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa baina ya watendaji wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, watendaji wa uchaguzi ngazi ya Mkoa wameaswa kutekeleza majukumu yao kwa ukaribu na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili kupata ufafanuzi na maelekezo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Mkoa wa Lindi unatarajiwa kuanza zoezi la Uandikishaji Daftari la Mpigakura kuanzia Januari 28 hadi Februari 03 mwaka huu ambapo wapigakura wapya 121,887 wanatarajiwa kuandikishwa na kufanya idadi kamili ya wapigakura kwa mwaka 2025 kufikia 768,641.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.