WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ATANGAZA KUTOGOMBEA TENA UBUNGE RUANGWA BAADA YA MIAKA 15 YA UTUMISHI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, leo Julai 2, 2025, ametangaza rasmi kutogombea tena nafasi ya ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu ujao, baada ya kulitumikia kwa kipindi cha miaka 15.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Ruangwa kwa kumuunga mkono na kushirikiana naye katika kipindi chote cha uongozi wake tangu mwaka 2010.
“Umefika wakati kwa mshikamano tulioujenga sasa ni wakati wa kutoa fursa kwa Wana-Ruangwa wengine wapenda maendeleo waweze kuunganisha nguvu hizi ili kaulimbiu yetu ya Ruangwa kwa Maendeleo Inawezekana iweze kusonga mbele zaidi,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya kuwapa ushirikiano wagombea wote watakaojitokeza kuwania ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akisistiza umuhimu wa kudumisha mshikamano na utulivu wakati wa mchakato wa kisiasa.
Katika salamu zake kwa wananchi, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi Wana-Ruangwa kuendelea kushikamana na kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni, kusikiliza sera za wagombea, na hatimaye kuwachagua kwa kura za kutosha wagombea wa CCM, akiwemo Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Vilevile, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wakuu wa CCM kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kulitumikia jimbo la Ruangwa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Kassim Majaliwa alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Ruangwa mwaka 2010, na tangu wakati huo ameendelea kuwa mhimili wa maendeleo na mshikamano katika jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 15.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.