ZAIDI YA AJIRA 100,000 KUZALISHWA WILAYANI KILWA KUTOKANA NA MRADI WA MIHOGO
Siku moja baada ya kutangaza mikakati nane (8) inayolenga kukuza uwekezaji nchini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Novemba 29, 2025 amemkabidhi Mwekezaji Pan Tanzania Agriculture Development eneo la mradi lililopo Kilwa, Mkoani Lindi.
Prof. Mkumbo amemkabidhi mwekezaji huyo eneo lenye ukubwa wa hekari 62,000 ambapo atatekeleza mradi wa kilimo cha mihogo, ujenzi wa viwanda vya uchakataji, na kuzalisha Unga kwa lengo la kuuza nje.
Akikabidhi mradi huo, Mhe. Prof. Mkumbo amesema kuwa mradi huo unakidhi vigezo vitano vya kuchagua sekta za kimageuzi, ambavyo pia ni vigezo vya kuchagua aina ya uwekezaji utakaopewa kipaumbele kama vinavyopendekeza Dira 2050.
Alitaja vigezo hivyo kuwa ni:
1. Uwezo wa mradi kuzalisha ajira: Mradi unazalisha zaidi ya ajira 100,000.
2. Uwezo wa mradi kuongeza mapato ya nje: Utachakata mihogo na kuuza unga nje ya nchi.
3. Uwezo wa mradi kuongeza thamani: Mwekezaji atalima na kuchakata, akiongeza thamani ya zao. 4. Kigezo cha kuleta ujuzi: Mradi unatarajiwa kuwajengea uwezo wakulima wa zao la mihogo zaidi ya 10,000.
5. Uwezo wa mradi kuchagiza sekta nyingine: Unategemea kujenga viwanda vya kuchakata bidhaa na kuleta mtaji wa nje unaokadiliwa kufikia Dola za Marekni bilioni 640.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji Sekta Binafsi, Bw. Aristides Mbwasi, alitoa salamu za Katibu Mkuu, Dkt. Tausi M. Kida, amesema kuwa makabidhiano hayo yanaashiria hatua muhimu katika safari ya Tanzania ya kubadilisha kilimo kuwa sekta ya kisasa, yenye ushindani, na inayoendeshwa na uwekezaji.
"Mkataba huu wa Maendeleo ya Ardhi unawakilisha utayari wetu wa kushirikiana na washirika wa kimkakati ambao huleta teknolojia, mtaji, na utaalamu ambao utainua jamii za wenyeji," amesema Bw. Mbwasi.





Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.