Katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi imeokoa kiasi cha zaidi ya Milioni 201 katika mradi wa ujenzi wa bandari ya Uvuvi Wilayani Kilwa pamoja na malipo ya wakulima wa ufuta Wilaya ya Lindi.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Lindi, Bwana. Justine Maingu ameeleza kwamba fedha hizo zimeokolewa kwa kufanya ufatiliaji wa miradi 6 ambayo iligundulika kuwa na mapungufu hafifu hivyo TAKUKURU Mkoa wa Lindi ikashauri mamlaka husika ili ziweze kufanya marekebisho ya mapungufu hayo.
Bwana. Maingu amebainisha kuwa kufuatia ufuatiliaji huo TAKUKURU Mkoa wa Lindi ilibaini kuwa mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko na kubaini Mkandarasi anayetekeleza mradi huo kutolipa ushuru wa huduma (Service Levy) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na kwamba kwa hatua zilizochukuliwa kiasi cha Shilingi 175,163,798.58 kiliokolewa na kuweza kulipwa kwa halmashauri ya Wilaya hiyo.
Aidha,ameeleza kuwa kutokana na malalamiko ya wakulima wa ufuta kutoka Chama cha Msingi cha Ushirika cha Ruhokwe (Ruhokwe Amcos) kuhusu ubadhirifu wa fedha za mauzo ya zao hilo kwa msimu wa mwaka 2023/2024 uliofanywa na baadhi ya viongozi wa matawi ya chama hicho wamefanikiwa kuhakikisha kiasi cha Shilingi 26,265,830.00 kinarejeshwa na baadhi ya viongozi wa matawi.
TAKUKURU Mkoa wa Lindi imeendelea kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao wanaouonyesha kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uwepo wa vitendo vya rushwa na kuwataka kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa hususan katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye kampeni na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Vilevile, Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Lindi ameeleza kuwa Taasisi itaendelea kutumia mbinu za matumizi ya TEHAMA, na za ana kwa ana pamoja na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU Rafiki ili kuweza kuongeza uelewa na kubadili mtazamo wa wananchi katika kuzuia na kupambana na rushwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.