ZIARA MAALUM YA KUKAGUA MRADI WA UFUGAJI WA SAMAKI YAFANYIKA KWA MAFANIKIO RUANGWA
Timu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu, ikiambatana na Afisa Uvuvi wa Mkoa wa Lindi, Ndugu Jumbe Kawambwa, imefanya ziara katika Vijiji vya Nahanga na Chikoko wilayani Ruangwa kwa ajili ya kufanya tathmini ya maendeleo ya mradi wa ufugaji wa samaki kwa wakulima wadogo. Mradi huo, unaotekelezwa kupitia programu ya ARNSA chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ufadhili wa NORAD kupitia IFAD, umejikita kuwawezesha wakulima wadogo kuongeza lishe, kipato na usalama wa chakula kwa kuwapatia mafunzo, vifaa na mbinu bora za ufugaji wa kisasa.
Tathmini ya awali imeonesha kuwa mradi umekuwa na mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Ruangwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa Uvuvi wa Mkoa wa Lindi, Ndugu Jumbe Kawambwa, amesema ziara hiyo imelenga kufuatilia utekelezaji wa mradi na kusikiliza changamoto zinazowakabili wanufaika.
“Tumefika hapa kuangalia maendeleo na kusikiliza changamoto mnazokutana nazo katika utekelezaji wa mradi huu, na kuona namna ambavyo mnanufaika na matokeo kama ilivyotarajiwa na serikali” amesema Kawambwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi, Ndugu Godfrey Christopher amewapongeza wakulima kwa kuendesha shughuli za ufugaji kwa ufanisi na kwa kuonesha juhudi ambazo zimekuwa msingi wa mafanikio yaliyopatikana.
“Nawapongeza sana. Mmefanya kazi kubwa hadi mlipofikia. Sisi tupo pamoja nanyi wakati wote, hivyo msisite kutupa taarifa za changamoto mnazopitia. Tunatarajia kuona mafanikio makubwa zaidi kupitia mradi huu” ameeleza.
Bi. Hatia Nunguye, mkazi wa Kijiji cha Nahanga, Kata ya Mandawa kwa niaba ya wafugaji wenzake ameishukuru serikali kwa kuwawezesha kupitia mradi huu ambao umesaidia kuboresha lishe na kuongeza kipato kutokana na mavuno mazuri ya samaki.
“Tunashukuru sana kwa huu mradi. Sasa tunapata lishe bora, na tumekuwa tukivuna samaki wengi ambao tunauza na kupata kipato” amesema Bi. Hatia.




Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.