SEKTA YA UVUVI KWA MKOA WA LINDI.
1. Utangulizi.
Sekta ya uvuvi kwa Mkoa wa Lindi inajumuisha shughuli za uvuvi wa samaki katika vyanzo vya maji vya asili (bahari, mito, na mabwawa), shughuli ya ufugaji wa samaki na kilimo cha mwani. Kwa upande wa vyanzo vya asili Mkoa umepitiwa na Bahari ya Hindi, Mto Lukuledi, Ziwa dogo la Rutamba na Mabwawa.
2. Shughuli ya uvuvi wa samaki.
Mkoa wa Lindi una mwambao wa bahari usiopungua urefu wa km 285 kutoka Kijiji cha Sudi (Kusini mwa Wilaya ya Lindi) mpaka Kijiji cha Marendego (Kaskazini mwa Wilaya ya Kilwa). Ukanda huu wa Bahari una fukwe nyingi zinazofaa kwa ukuzaji wa viumbe vya majini kama vile samaki, kaa, chaza na kilimo cha Mwani.
Ukanda huu ndio wenye jamii inayojishughulisha na uvuvi wa samaki kwa kiasi kikubwa kutokana na uwepo wa bahari ambapo unaojumuisha Wilaya za Lindi na Kilwa. Uvuaji samaki hufanywa kwa kutumia zana na teknolojia mbalimbali (kama madema, wando, zurumati, mishipi ya mkononi, nyavu ndogo za jarife, nyavu za kilindini za kuzungusha makundi ya samaki, vimia na nyavu za dagaa) kulingana na aina tofauti za samaki wanaoruhusiwa kuvuliwa kwa mujibu wa sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009, sera ya uvuvi na miongozo mbalimbali.
Vyombo vinavyotumika kuvulia ni mashua, madau, ngalawa na mitumbwi (dugout cones) vinavyoendeshwa ama kwa kutumia matanga (upepo) au makasia.
Baadhi ya aina ya samaki wanaopatikana
Shughuli za usimamizi raslimali za uvuvi.
Shughuli ya usimamizi na udhibiti uvunaji raslimali za bahari unafanywa na vyombo mbalimbali vya serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Halmashauri za Wilaya zote tatu zinawajibika katika kuhifadhi na kusimamia uvunaji endelevu wa raslimali za uvuvi. Pia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kupitia vituo vyake vya doria vilivyoko Wilaya ya Kilwa na Wadau mbalimbali kama WWF wanashirikiana na Mkoa katika usimamizi wa rasilimali hizi.
Halmashauri zimeunda na zinaendelea kuunda vikundi shirikishi vya usimamizi raslimali uvuvi (Beach Management Unit, BMUs) katika vijiji na mataa ya jamii ya uvuvi.
3. Ufugaji wa samaki.
Hii ni shughuli inayofanyika katika maeneo mbalimbali ya Mkoa ambayo yana vyanzo vizuri vya maji baridi na maji chumvi. Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale shughuli za ufugaji wa samaki zinafanyika katika vyanzo vya maji baridi na aina ya samaki wanaofugwa ni perege na kambale.
Zaidi ya hekta 10 kwa Mkoa wa Lindi zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji kutokana na uwepo wa mabonde ya maji yanayotiririsha maji mwaka mzima. Hivyo maeneo hayo ni fursa pia kwa ufugaji wa samaki wa maji baridi ambapo shughuli hiyo inaweza kufanywa kwa pamoja na kilimo.
Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Manispaa ya Lindi na Kilwa ufugaji wa samaki unafanyika katika pwani ya bahari na maeneo ya vyanzo vya maji baridi. Aina ya samaki wanaofugwa katika maeneo ni kambale, mwatiko, perege na kaa.
4. Kilimo cha mwani.
Mwani ni mimea inayoota kwenye maji, na mingine huota na kuishi katika maji chumvi na mingine katika maji baridi (mito, maziwa nk). Mfano mimea ya nchi kavu ina mizizi kwa ajili ya kufyonzea maji na chumvi ardhini, ina mashina na pia ina majani, lakini mimea aina ya mwani haina mizizi, majani wala shina, hivyo ufyonzaji wa chakula hufanywa na sehemu zote za mmea mzima.
Aina za mwani.
Kwa Mkoa wa Lindi hii ni shughuli ya kilimo inayafanywa na jamii ya pwani ya bahari ambapo shughuli hiyo hufanyika ndani ya bahari.
Uwepo wa bahari Mkoani Lindi ni fursa pekee kwa wakazi wa mwambao wa pwani katika kukuza na kuendeleza kilimo cha mwani na kuweza kujiongeza kipato. Kama ilivyo shughuli ya uvuvi, kilimo cha mwani kinafanyika katika Halmashauri za Wilaya ya Kilwa, Lindi na Manispaa ya Lindi huku aina mbili za mwani cotonii na syprosum zikiwa zinalimwa kwa wingi.
Pamoja na uwepo wa bahari katika Mkoa wa Lindi uzalishaji wa zao la mwani umekuwa ukishuka kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali hasa kushuka kwa bei ya zao hilo sokoni na magonjwa yanayoshambulia zao hilo.
Mkoa unaendelea kuhamasisha wakulima wa mwani kuuchakata mwani kwa lengo la kuuongezea thamani pamoja na kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na mwani. Pia Mkoa kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Rasilimali Uvuvi ya TAFIRI unaendelea na tafiti mbalimbali zikiwemo za magonjwa yanayolikabili zao la mwani.
5. CHANGAMOTO NA MIKAKATI YA KUKABILIANA NAZO.
5.a. Changamoto
Pamoja na mafanikio mengi yaliyopatikana, Mkoa unakabiliwa na changamoto zifuatazo kupitia Sekta ya uvuvi:-
5.b. Mikakati
Ili kufikia malengo yaliowekwa katika kuendeleza sekta ya uvuvi kwa ujumla na kutokana na hali halisi ya sekta ya Uvuvi katika Mkoa wetu ukilinganisha na changamoto zilizopo kwenye Halmashauri zetu, Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM) hazina budi kusimamia na kuendeleza rasilimali za Uvuvi kwa kuzingatia mambo yafuatayo: -
Kurudisha asilimia (15%) kutoka kwenye makusanyo ya ndani kupitia sekta ya uvuvi ili ziweze kusaidia kuendeleza sekta.
Kuona uwezekano wa kuvipatia vikundi vya Usimamizi wa rasilimali za uvuvi uwakala wa kukusanya mapato ili viweze kuwa endelevu.
Kuandika maandiko ya kuomba fedha kutoka vyanzo mbalimbali na kubuni mbinu nyingine zinazoweza kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya kuendeleza sekta ya uvuvi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.