MAELEZO NA HISTORIA KUHUSU MKOA WA LINDI
Historia ya Mkoa wa Lindi
Mwaka 1961 wakati Tanganyika inapata Uhuru wake kutoka kwa Waingereza Mkoa wa Lindi haukuwapo kabisa katika ramani. Kilichokuwapo wakati huo ni Jimbo la Kusini ambalo lilijumuisha Mikoa ya sasa ya Lindi Mtwara na Ruvuma. Makao Makuu ya Jimbo hilo la Kusini yalikuwa katika Mji wa Lindi.
Hadhi ya Mji wa Lindi kuwa Makao Makuu iliishia mara baada ya Uhuru ambapo Jimbo la Kusini likawa linajulikana kama Mkoa wa Mtwara. Makao Makuu yakawa ni Mji wa Mtwara. Yamkini Mkoa wa Mtwara ulikuwa mkubwa sana kwa eneo hata Mkuu wa Mkoa wa kwanza wa Mtwara Bwana John Nzunda alikuwa anasema:
“Natawala kipande cha nchi toka Pwani ya Bahari ya Hindi hadi Ziwa Nyasa na kutoka Mto Ruvuma hadi karibu na mto Rufiji.”
Serikali wa awamu ya kwanza Iliyoongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliugawa Mkoa wa Mtwara miaka ya mwanzo ya Uhuru ambapo kukawa na Mikoa ya Mtwara na Ruvuma. Mgawanyiko huu uliifanya Lindi kuwa ndani ya Mtwara.
Julai 1, 1971 ndipo Mkoa wa Lindi ulianzishwa rasmi baada ya tena kuugawa Mkoa wa Mtwara. Makao Makuu ya Mkoa yakawa Mji wa Lindi. Wakati Tanzania inaadhimisha Miaka 10 ya Uhuru wa Bara kwa kuwaita Waingereza kuja kuiona hatua iliyopiga Mkoa ulikuwa na umri wa miezi 6 tu.
Eneo
Mkoa wa Lindi unapakana na Bahari ya Hindi upande wa Mashariki, Mkoa wa Pwani upande wa Kaskazini, Morogoro na Ruvuma upande wa Magharibi na upande wa Kusini ni Mkoa wa Mtwara.
Mkoa una eneo la kilometa za mraba 67,000 ambalo ni sawa na asilimia 7.1 ya eneo la Tanzania Bara. Hata hivyo karibu asilimia 27 ya eneo la Mkoa lipo chini ya mbuga ya Selous (Selous Game Reserve) ambayo iko Magharibi mwa Wilaya ya Liwale.
Utawala
Mwaka 1971 Mkoa wa Lindi ulianza ukiwa na Wilaya 3 – Lindi, Kilwa na Nachingwea. Wilaya ya Liwae ilianzishwa kwa kuigawa Wilaya ya Nachingwea mwaka 1975 na Ruangwa ilianzishwa mwaka 1995 kwa kuigawa Wilaya ya Lindi. Zipo Halmashauri 6 ambazo ni Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Halmashauri za Wilaya za Lindi, Kilwa, Nachingwea, Liwale na Ruangwa.
Pia Mkoa una jumla ya Tarafa 28, Kata 152, Mitaa 117, Vijiji 526 vilivyoandikishwa, Miji Midogo 3, (Kilwa Masoko, Kilwa Kivinje na Nachingwea), vitongoji 2,429 na Majimbo 8 ya Uchaguzi na Wabunge wa Viti Maalum 2.
Kwa wastani hali ya hewa katika Mkoa huu ni ya joto la kati ya nyuzi joto 24C hadi 27C na joto hili hutegemea sana pepo za bahari zinazovuma katika kipindi husika kwa mfano pepo za Kusi ni za baridi na Kaskazi huleta joto. Sehemu za miinuko zilizoko kati na Kaskazini kama Rondo, Kilimarondo, Kipatimu na Mpigamiti hali ya joto hupungua na kuonyesha tofauti za nyakati za joto na baridi.
Mvua
Mvua hunyesha mwezi Novemba mpaka Aprili na hali ya ukame kati ya Januari na Februari, Agosti hadi Oktoba. Wastani wa mvua kwa mwaka ni Milimita 750 – 1,200.
Idadi ya Watu
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Mkoa wa Lindi una jumla ya wakazi 864,652 wanaume wakiwa 414,507 na wanawake 450,145.
Mkoa una makabila mbalimbali ambayo ni Mwera, Makonde, Ngindo, Matumbi, Machinga, na watu wachache wenye asili ya Asia na Kiarabu.
Dini
Mkoa wa Lindi una Dini zifuatazo: Wakristo 30%, 45% Muslem, Hindu 0.01% wengine 24.09%
Uchumi
Uchumi wa Mkoa wa Lindi unategemea sana sekta ya kilimo ambayo asilimia kubwa ni kilimo cha kujikimu na biashara kiasi. Hata hivyo vipo vyanzo vingine vya kiuchumi ambavyo ni Uvuvi, Ufugaji nyuki na Mifugo, Madini, Viwanda vidogo na vya Kati.
Huduma za Jamii
Mkoa unatoa huduma za jamii (ambazo ni Afya, Elimu, Maji, Utamaduni na Michezo) katika Mkoa utoaji wa huduma hizi umeendelea kupanuka kulingana na malengo ya serikali ya kuwasogezea wananchi huduma mahali walipo. Changamoto iliyopo ni ufinyu wa bajeti lakini Mkoa unaendelea kutoa huduma bora na kwa viwango vinavyostahili.
Mawasiliano Na Uchukuzi
Mawasiliano, Huduma za posta, Telefax, Internet na Telex zinapatikana katika miji yote iliyotajwa hapo juu. Kwa upande wa usafiri Mkoa umeunganishwa na Wilaya zake zote kwa barabara zenye jumla ya kilomita 7,118 kati ya hizo kilomita 1200 ni za lami.
Mkoa una Bandari maji mbili za Lindi na Kilwa, bandari ya Lindi kwa sasa ipo katika matengenezo lakini ya Kilwa inaendelea kufanya kazi. Kwa upande wa viwanja vya ndege kipo kiwanja chenye barabara 6 ambacho sio cha lami. Kilwa na Nachingwea vipo viwanja vyenye barabara moja. Liwale kipo kiwanja cha kutua ndege ndogo.
Pato la Mkoa
kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2009 Pato la mkazi kwa mwaka lilikuwa shilingi 767,948 na mwaka 2015 liliongezeka na kufikia shilingi 1,901,044 hili ni ongezeko la asilimia 148 kwa wastani wa ongezeko la asilimia 21 kwa mwaka. Pia pato la Mkoa limeendelea kuongezeka kutoka shilingi 695,361,000 mwaka 2009 hadi kufikia shilingi 1,690,403,000 mwaka 2015, hili ni ongezeko la silimia 143 kwa wastani wa silimia 20 kwa mwaka. Pamoja na kuwepo kwa ongezeko hilo la kipato bado kumekuwepo na changamoto kubwa ya umaskini miongoni mwa wananchi, hivo basi Serikali ya Mkoa inaendelea na jitihada za kuwahamasisha wananchi wote wenye uwezo wa kufanya kazi wafanye kazi ili kuendana na kauli mbiu ya “HAPA KAZI TU”.
JEDWALI NA. 3: PATO LA MKAZI NA PATO LA MKOA KWA KIPINDI CHA 2009 – 2015
Pato la Mkazi kwa mwaka (per capita) |
Pato la Mkoa kwa mwaka(GDP) (000) |
|
2009 |
767,948 |
695,361 |
2010 |
913,678 |
843,880 |
2011 |
1,061,282 |
999,604 |
2012 |
1,341,117 |
1,159,599 |
2013 |
1,503,942 |
1,312,577 |
2014 |
1,677,336 |
1,482,763 |
2015 |
1,901,044 |
1,690,403 |
Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS, 2016).
NB: Takwimu hizi zinaonyesha kwamba, kwa wastani wananchi wa Mkoa wa Lindi, wamevuka kiwango cha umaskini uliokithiri cha watu kuishi chini ya dola moja kwa siku.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.