Mkoa wa Lindi kihistoria sio wa kiufugaji, wafugaji wachache waliopo hufuga zaidi mbuzi, kondoo, kuku, bata, kanga, njiwa na ng’ombe kwa uchache sana. Mara nyingi hutumiwa kwa kitoweo, shughuli za biashara, kimila na utamaduni. Hivyo, Mkoa wa Lindi una mifugo michache ukilinganisha na Mikoa mingine ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Nyanda ya Juu Kusini. Hata hivyo, sekta ya mifugo Mkoani Lindi imeendelea kukua baada ya Serikali ya Mkoa kukubali kupokea mifugo toka Mikoa mingine yenye ng’ombe wengi na mwamko unaoongezeka wa wakazi wa Mkoa wa Lindi katika kujiletea maendeleo yao kupitia sekta ya mifugo.
HALI YA UCHUMI NA MCHANGO WA SEKTA YA MIFUGO KATIKA UCHUMI WA MKOA
Wananchi wengi wa Mkoa wa Lindi wanategemea kuendesha maisha yao ya kila siku kwa kutegemea shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi. Mifugo hii inachangia kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, Halmashauri na Mkoa kwa ujumla kama ifuatavyo;
Huboresha afya za wanachi kwa kuwa ndio chanzo kikuu cha uto mwili (protein) inayotokana na ulaji wa nyama, maziwa na mayai.
Usalama wa chakula – Mifugo hutumika kama rasilmali hivyo kunapokuwa na upungufu wa aina zingine za vyakula vya nafaka mifugo huuzwa ili wananchi wanunue hivyo vyakula.
Huchangia pato la Halmashauri husika- Mchango wa mifugo katika Halmashuri unatokana na ushuru wa machinjio, leseni za wafanyabiashara wa nyama, ushuru unaotokana na usafirishaji wa mifugo n.k.
Biashara ya mifugo na mazao huchungia mzunguko wa fedha katika Mkoa. Mfano kwa kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi 2018 fedha zilizotokana na bishara ya mifugo katika Halmashauri zote Mkoani Lindi ni zaidi ya shilingi 5,103,759,294.91 za kitanzania.
IDADI YA MIFUGO
Mkoa wa Lindi hadi kufikia mwezi Machi, 2018 una jumla ya Ng’ombe wa asili 118,760, Mbuzi asili 79,183, Mbuzi wa kisasa 8,138, na Kondoo 9,007. Mifugo mingine ni Ngamia 10, Nguruwe 5,166, Mbwa 14,488, Kuku 1,460,491, Punda 121, Kanga 5,788, Bata 25,111, Bata mzingi 112, Paka 7,627, Njiwa 1,586 na Sungura 212. Jedwali lifuatalo linaonesha hali halisi ya ukuaji wa sekta ya Mifugo Mkoani Lindi tangu mwaka 2003/04 hadi mwaka 2017/18
Ukuaji wa Sekta ya Mifugo Mkoani Lindi
Mwaka
|
2003/04
|
2012/13
|
2017/18
|
Ng'ombe
|
12,000
|
40,461
|
118,760
|
Mbuzi
|
34,500
|
76,088
|
87,321
|
Kondoo
|
12,900
|
12,742
|
8,736
|
Nguruwe
|
2,400
|
5,221
|
5,166
|
Mbwa
|
11,280
|
15,593
|
14,488
|
Kuku
|
16,890
|
1,700,576
|
1,460,491
|
Punda
|
-
|
108
|
121
|
Bata
|
3,760
|
94,962
|
25,223
|
Paka
|
2,670
|
5,673
|
7,627
|
Sungura
|
-
|
110
|
212
|
Ngamia
|
-
|
-
|
10
|
Njiwa
|
200
|
760
|
1,586
|
UENDELEZAJI WA MIUNDO MBINU YA MIFUGO
Eneo lililotengwa kwa ajili ya malisho.
Halmashuri za Wilaya za Nachingwea, Kilwa, Liwale na Lindi zilikwishatenga maeneo ya kupokea wafugaji kutoka mikoa mingine. Ni Vijiji 59 ambavyo vimeshawekewa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi na kutenga maeneo kwa ajili ya malisho ya mifugo. Maeneo yote yaliyotengwa yana jumla ya hekta 293,909.69 yenye uwezo wa kutoa malisho kwa idadi ya mifugo ipatayo 146,955.Halmmashauri za Mkoa Lindi zinaendelea na zoezi la kutenga zaidi maeneo mengine kwa ajili ya kupokea mifugo pamoja na kuimarisha miundo mbinu katika maeneo hayo.
Aidha, katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji lakini kuna mifugo inayotegemea malisho ipatayo 13,589 na 16,529 kwa mfuatano huo.
Malambo/Mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo
Jumla ya malambo na mabwawa yaliyopo katika Mkoa ni 13 ambapo kati ya hayo yanayofanya kazi ni 6, mabovu/yaliyojaa tope ambayo yanayohitaji kufanyiwa ukarabati ni 6 na moja halifanyi kazi.
Majosho
Mkoa una jumla ya majosho 19 ambapo majosho yanayofanya kazi ni 6, majosho mazima yasiyofanya kazi ni 2, mabovu yanayohitaji ukarabati ni 10, na josho moja ni binafsi. Aidha, majosho mengi yameshazungukwa na makazi ya watu hivyo hayafai kutumika kwa mfano katika halmashauri ya Nachingwea.
Mashamba ya Mifugo yaliyopo Mkoani Lindi
Katika Mkoa wa Lindi yapo mashamba 7 ya mifugo ambapo shamba la Mtanga linamilikiwa na Jeshi la Magereza lipo Wilaya ya Kilwa na linafanya kazi, Shamba la Narunyu linamilikiwa na Narunyu Sister’s Convent lipo Wilaya ya Lindi na linafanya kazi, Shamba la Magereza Kingurungundwa linalomilikiwa na Jeshi la Magereza lipo vizuri na linafanya kazi, Shamba la Mayola linalomilikiwa na Ally Mayola lipo Manispaa ya Lindi na Linafanya kazi na Shamba la L.M.U. Farm III linalomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea ambapo uzalishaji wake ni mdogo hivyo linahitaji uwekezaji mkubwa na shamba moja la mfugaji Mkubwa katika kijiji cha Matekwe Halmashauri ya Nachingwea.
Idadi ya minada iliyopo na inayofanya kazi
Mkoa wa Lindi una jumla ya minada minne (4) kati ya hiyo, miwili inapatikana Kilwa, Manispaa ya Lindi ina mnada mmoja ambao haufanyi kazi na Halmashauri ya Lindi ina mnada mmoja uliokuwa unafanya kazi. Aidha, katika Halmashauri za Liwale, Nachingwea na Ruangwa hakuna minada na juhudi zinafanyika ili kuwa na minada katika Halmashauri hizo.
Kituo cha uhamilishaji kinavyofanya kazi.
Katika juhudi za kuendeleza shughuli za uhimilishaji nchini, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeanzisha kituo cha uhimilishaji cha kanda ya kusini kilichopo Mkoani Lindi. Kituo hiki kipo ndani ya eneo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi na kilifunguliwa rasmi Oktoba 2012. Pamoja na shughuli nyingine kituo hiki kimesimikwa Mtambo wa kuzalisha kimiminika cha hewa baridi ya Naitrojeni ambayo hewa hii hutumika kama pembejeo muhimu ya kuhifadhi mbegu za madume bora na chanjo.
Wizara imejenga kituo hiki ili kukidhi mahitaji ya pembejeo hiyo muhimu kwa wataalamu na wadau wengine wanaofanya shughuli ya uhimilishaji na chanjo kwa wafugaji wanaoishi kwenye mikoa ya kanda ya kusini hususani Lindi, Mtwara na Ruvuma, hivyo kuwapunguzia wataalamu wa uhimilishaji mzigo wa gharama ya kusafiri umbali mrefu kufuata kimiminika hiki muhimu cha naitrojeni cha kuhifadhia mbegu na chanjo Kibaha Mkoani Pwani. Hadi mwezi Machi, 2018 jumla ya ng’ombe 112 wamehimilishwa na ng’ombe wengine 110 wanategemewa kuhimilishwa kuanzia mwezi wa Aprili, 2018
Huduma Zitolewazo na kituo
Kuzalisha hewa baridi ya kimiminika cha naitrojeni na kuuza kwa Taasisi na sekta binafsi.
Kuuza Mbegu za madume bora kutoka Kituo cha Taifa cha uhimilishaji kilichopo Usa River, Arusha (NAIC)-Mbegu bora za ngombe wa maziwa na nyama.
Kuuza Vitendea Kazi vya uhimilishaji.
Kusimamia, kufuatilia na Kutoa taarifa ya uhimilishaji Wizarani na Kituo cha taifa cha uhimilishaji kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara.
MAGONJWA YANAYOSUMBUA MIFUGO
Kuna magonjwa mengi yanayosumbua mifugo Mkoani Lindi kulingana na aina ya mifugo. Kwa upande wa ng’ombe kuna magonjwa makubwa matatu ambayo yanasababisha vifo kwa wingi. Kwanza, ugonjwa wa mapafu (CBPP), Ndorobo (Trypanosomiasis) na minyoo (Helminthosis). Kwa upande wa kuku ni Kideri, Kuhara damu (Coccidiosis), Minyoo na Fowl typhoid (Homa ya matumbo).
Mbuzi na kondoo wanasumbuliwa sana na Kuharisha (Enteritis) na Minyoo (Helminthosis). Kwa miaka mingi magonjwa haya hayakuwepo kutokana na kutoingizwa kwa mifugo kulikosababishwa na hali ya kijografia hasa kuwepo kwa mto Rufiji upande wa kaskazini, mto Lemusule upande wa Magharibi, mto Ruvuma upande wa kusini na bahari ya Hindi upande wa mashariki, hivyo ilikuwa vigumu kwa wafugaji kuingiza mifugo kwa wingi.
Hivyo, Mikoa ya Lindi na Mtwara ikawa ni ukanda huru wa magonjwa ya mifugo (Animal Disease Free Zone), lakini baada ya kukamilika kwa barabara ya Kibiti – Mingoyo kwa kiwango cha lami na ujenzi wa daraja la Mkapa katika mto Rufiji uingiaji wa mifugo umeongezeka kwa kiasi kikubwa sana na hivyo kuleta magonjwa ambayo hayakuwepo awali.
Hali ya madawa na usambazaji wake.
Hali ya madawa ya mifugo Mkoani Lindi si yakuridhisha kutokana na historia ya mkoa kuwa si wa wafugaji, hivyo kuna maduka machache sana ya pembejeo na madawa za mifugo. Mengi ya maduka haya yapo Manispaa ya Lindi ambako yapo maduka matano tu na kila halmashauri kuna duka moja moja, hivyo, kuna fursa kubwa ya biashara ya madawa ya mifugo na pembejeo zake.
MAZIWA NA MAYAI YALIYOZALISHWA NA THAMANI YAKE
Katika Mkoa wa Lindi maziwa yanayozalishwa kwa siku ni lita 11,389 ambapo lita moja hununuliwa kwa bei ya shilingi 1000 - 2000. Kwa upande wa mayai huzalishwa wastani wa mayaai 7,300 kwa siku ambapo yai moja huuzwa kwa wastani wa shilingi 400 hadi 500. Asilimia 95 ya mayai hutokana na kuku wa asili na kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mayai hutegemea sana toka Mikoa ya Pwani na Dar -es -Salaam, hivyo ipo fursa kubwa ya uwekezaji hususani katika ufugaji wa kuku wa mayai.
Ufugaji wa kuku na uzalishaji wa mayai
Mkoa wa Lindi una fursa kubwa ya kuwazalisha kuku wengi kwa ajili ya biashara na kuboresha afya ya wananchi kupitia nyama yake na mayai. Hadi sasa hakuna wazalishaji wakubwa wa kuku wa mayai, wafugaji walipo ni wadogo ambao hufuga kuku wasiozidi 20 hasa wa kienyeji. Kutokuwepo kwa wazalishaji wa mayai kumepelekea bei ya trei moja la mayai kuuzwa kwa shilingi 11,000 kwa yale ya kisasa na shilingi 15,000 kwa mayai ya kienyeji.
Aidha, mwezi Februari, 2018 Ofisi ya Mkuu wa mkoa ilipokea barua toka Wizara ya Mifugo na uvuvi ikitambulisha mradi wa uzalishaji wa kuku hususani aina ya Kuroiller unaofadhiliwa na Bill and Melinda Gates Foundation kwa kipindi cha miaka minne kuanzia januari 2018 hadi Januari 2021 na kutekelezwa na Kampuni ya AKM Glitters Ltd ya Dar es Salaam . Aidha, Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri wamejulishwa kuhusu mradi huu na taarifa hizi tayari zilishawafikia wananchi.
Hadi kufika tarehe 31 Machi, 2018 mawakala wawili walipatikana na kuletewa vifaranga vya siku moja 1737 pamoja na vyombo vya chakula, maji na mchanjo. Huduma ya ugani imetolewa ipasavya na Mgani wa Kampuni AKM Glitters. Mawakala wengine watatu wameletewa vifaranga 5940 mwezi Aprili na Mei, 2018. Jumla ya vifaranga vya Kuroiller walioingizwa mkoani Lindi kwa miezi mitatu tangu mradi huu umeanza ni 7677.
Ni matumaini ya Mkoa kuwa mara baada ya halmashauri zetu kuwahamasisha wananchi ufugaji wa kuku utakuwa mkubwa hususan aina hii ya Kuroiller ambao hutaga mayai kuanzia 150 hadi 200 kwa mwaka ukilinganisha na kuku wa kienyeji wanaotaga mayai 40 hadi 50 kwa mwaka. Aidha, aina hii ya kuku hukua haraka na madume hufikia uzito wa kilo 3.5 na majike kilo 2.5 hivyo wataongeza upatikanaji wa mayai na nyama ya kuku na kuweza kuboresha afya ya wananchi.
Kuroiller Kuroiller wakiwa Mtanda, Lindi Manispaa
Ulaji wa mazao yatokanayo na mifugo.
Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa, wastani wa taifa wa ulaji nyama kwa mtu mmoja kwa mwaka ni kilo 12 lakini kwa Mkoa wa Lindi ni kilo 1.5. Kwa upande wa unywaji wa maziwa, wastani wa taifa ni lita 24.6 kwa mtu kwa mwaka wakati Mkoani Lindi ni lita 1.6 tu (tofauti ya lita takribani 23). Vilevile, takwimu zilizopo za ulaji wa mayai kitaifa ni mayai 26 kwa mtu kwa mwaka wakati kwa Mkoa wa Lindi ni wastani wa mayai 13. Katika uzani wa kimataifa, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa ulaji wetu kitaifa uko chini ya ule wa Africa
VIWANDA VYA KUSINDIKA MAZIWA
Mkoa wa Lindi hakuna viwanda vya kusindika maziwa badala yake kuna wasindikaji wadogo 5 wanaojihusisha na usindikaji wa maziwa Lindi mjini na shirika la masister wa Narunyu katika halmashauri ya Lindi kwa kiwango kidogo ambacho hakikidhi mahitaji.
IKAMA YA WATUMISHI WA SEKTA YA MIFUGO
Mkoa wa Lindi una jumla ya watumishi wa mifugo 113 wakati mahitaji ni watumishi 262 hivyo upungufu ni watumishi 148. Mkoa utaendelea kuajri watumishi ili kujaza nafasi kadri utakapopata vibali.
HUDUMA NYINGINE ZILIZOTOLEWA NA SEKTA YA MIFUGO
Sekta ya mifugo imekuwa ikitoa huduma mbalimbali zikiwemo za ushauri kwa wafugaji ili wafuge kisasa, Ukaguzi wa nyama zinazochinjwa na machinjio kwa ujumla, shughuli za ugani zimeendelea kutolewa katika ngazi za kata na vijiji na hii ni pamoja na ufuatiliaji wa magonjwa na utoaji wa kinga, kuhasi na upigaji chapa mifugo.
CHANGAMOTO NA MIKAKATI YA KUKABILI
Changamoto
Mikakati iliyopo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.