Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amezitaka Asasi Zisizo za Kiserikali (AZAKI) kujenga na kudumisha Ubia na serikali kwani inatambua mchango wa Asasi hizo katika kuwezesha Maendeleo ya Nchi.
Mhe. Ndemanga ameyasema hayo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe, Bi. Zainab Telack katika Mkutano wa Mwaka wa Asasi Zisizo za Kiserikali (AZAKI) katika Mkoa wa Lindi yenye kauli mbiu ya 'SERA NA MIONGOZO BORA INAYOTOLEWA NA SERIKALI NI UHAI WA AZAKI' uliofanyika leo Juni 24, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
"Serikali inatambua mchango na umuhimu wa kufanya kazi na mashirika yasiyo ya kiserikali na inatambua mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchi na mtu mmojammoja, kukuza na kuibua vipaji mbalimbali pamoja na kulinda haki za binadamu" Mhe. Ndemanga.
Aidha, Mkuu wa wilaya amesisitiza Uwazi na Uwajibikaji wa AZAKI katika shughuli mbalimbali wanazozifanya katika jamii na ndani ya taasisi ikiwemo Vyanzo vya mapato (Fedha) zinazopatikana na kutumika katika taasisi pamoja na kufanya kazi kwa kulinda maslahi ya nchi.
"Mkiwa wawazi mtaaminika na kupewa kazi na serikali lakini nisisitize kufanya kazi kwa kulinda maslahi ya nchi yetu, tusiingie katika matatizo ya kushirikiana na wafadhili wanaotoa fedha bila masharti ili uzipate kiurahisi na uende kinyume cha mila na desturi za jamii zetu tutasababisha vurugu na uvunjifu wa amani"
Asasi Zisizo za Kiraia pia zimetakiwa kutoa taarifa za shughuli zao kila robo ya mwaka pamoja na taarifa za upatikanaji wa fedha na matumizi yake ili kuondokana na shutuma za utakatishaji wa fedha pamoja na kufikisha misaada mbalimbali inayotolewa na wafadhili kwa walengwa kama ilivyopangwa ili kujijengea imani kwa wananchi wanaowahudumia
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.