Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shirika la maendeleo ya petrol nchini TPDC Balozi Ombeni Sefue amewataka wananchi wa mkoa wa Lindi kuchangamkia fursa ambazo zitaambatana na mradi wa uchakataji wa gesi asilia unaotarajiwa kujengwa katika eneo la Likong’o, Manispaa ya Lindi.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika jumamosi ya tarehe 27 Agosti 2022 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi Balozi. Ombeni Sefue amewataka wananchi wa Lindi kujiandaa na fursa nyingi zitakazozalishwa na mradi huo.
Balozi Sefue amesema kuwa haitakuwa vyema ikiwa fursa hizo zitachangamkiwa na watu kutoka nje ya Mkoa wa Lindi.
"Upande wa viongozi kuendelea kuwahamasisha wananchi kuanza kutambua fursa ambazo zinakuja na kujiandaa......ujenzi ukianza hapa, wakinunua kuku, wananunua kuku siku moja wote wanakwisha."
" Vijana wajue kwamba kunufaika ni lazima ujiandae na sio ujiandae tu ujiandae kwa viwango vya kimataifa." Amesema Balozi Sefue.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Telack amesema wananchi wa Mkoa wa Lindi wako tayari kuupokea mradi huo na wanasubiri kuanza kwa utekelezaji. “Sisi Lindi tuko tayari wakati wowote mradi utakapokuwa unaanza, eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo halina malalamiko, halina madai na wananchi wetu wanachosubiri ni kuona utekelezaji".
Akitoa taarifa fupi, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amesema kuwa kuelekea katika utekelezaji wa mradi huo mkubwa, Kwa sasa zoezi la uunganishaji miundombinu ya huduma ya gesi majumbani linaloratibiwa na Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania , TPDC liko kwenye hatua nzuri ambapo kwa awali zoezi hilo limeanza na nyumba zilizopo eneo la mnazi mmoja,manispaa ya lindi.
Katika kikao hicho, Balozi Ombeni Sefue aliambatana Wajumbe wa Bodi ya TPDC, Wakurugenzi na Watendaji wa Shirika hilo la Maendeleo ya Petrol kwa lengo kuu la kuitambulisha bodi hiyo tangu iteuliwe na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Mei 2022.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Lindi
Sanduku la Posta: P.o Box 1054 Lindi
Simu: 023-220-2098
Rununu:
Barua pepe: ras.lindi@tamisemi.go.tz
Hati miliki ©2017 Lindi . Haki zote zimehifadhiwa.